Iran na Qatar zasisitiza ulazima wa kuhitimishwa mauaji ya kimbari Ukanda wa Gaza

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Qatar katika mazungumzo yao mjini Tehran wamesisitiza juu ya ulazima wa kukomeshwa mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran jana alasiri alikuwa na mzungumzo na Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ambaye amefanya safari hapa Tehran akiongoza ujumbe rasmi wa nchi yake kwa ajili ya mashauriano kuhusu uhusiano wa pande mbili na matukio nyeti ya ya Magharibi mwa Asia.  

Katika mazungumzo hayo, pande mbili zimeashiria ulazima wa kukomeshwa mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza na kusitishwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon. Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani na Abbas Araqchi pia wamesisitiza kuendeleza mashauriano kati yao na kukusanya nguvu na suhula zote za kikanda na kimataifa ili kuzuia kuenea hali ya mchafukoge katika Asia Magharibi. 

Mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza 

Kadhalika, Sayyed Abbas Araqchi na Sheikh Mohammad bin Abdurrahman Al Thani wamechunguza pia baadhi ya masuala ya ushirikiano kati ya Iran na Qatar na kutilia mkazo juu ya kuendelezwa njia hiyo wakiashiria kustawi uhusiano wa nchi mbili katika nyanja zote.