
Marekani na Iran zinakutana nchini Oman siku ya Jumamosi kwa duru ya tatu ya mazungumzo muhimu kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, kufuatia mijadala ya awali iliyoelezwa kuwa yenye kujenga na nchi hizo mbili, maadui kwa miongo minne.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Mazungumzo haya, chini ya upatanishi wa Oman, yanafuatia mijadala isiyo ya moja kwa moja ambayo tayari ilifanyika Aprili 12 huko Muscat na kisha tarehe 19 huko Roma.
Tehran na Washington hazijakuwa na uhusiano wa kidiplomasia tangu mwaka 1980. Majadiliano haya ni ya kwanza katika ngazi hii tangu Marekani ilipojiondoa mwaka 2018, chini ya uongozi wa kwanza wa Donald Trump, kwenye makubaliano ya kimataifa yaliyohitimishwa miaka mitatu mapema ambayo yalidhibiti mpango wa nyuklia wa Iran kwa kubadilishana na kuondolewa kwa vikwazo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi na mjumbe wa Marekani kwa Mashariki ya Kati Steve Witkoff watafanya mazungumzo nchini Oman siku ya Jumamosi, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Badr al-Busaidi akikaimu kama mpatanishi, kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmail Baghai.
Kikao cha mazungumzo ya kiufundi kati ya wataalamu kinapangwa kabla ya mazungumzo ya ngazi ya juu. Mazungumzo hayo yataanza mwendo wa saa 8:30 asubuhi (sawa na saa 4:30), kwa mujibu wa televisheni ya taifa ya Iran, ambayo haikubainisha iwapo ungekuwa mkutano wa kiufundi au kati ya maafisa wa ngazi za juu.
Mkutano wa Aprili 19 ulielezewa kuwa “mzuri” na nchi zote mbili. “Ili mazungumzo yaendelee, lazima kuwe na onyesho la nia njema, umakini na uhalisia kwa upande mwingine,” Bw. Baghaï amesema Ijumaa.
– “Matumaini ya tahadhari” –
Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani na Israel zinashuku Iran kutaka kupata silaha za nyuklia. Tehran inakataa madai haya, ikitetea haki yake ya nishati ya nyuklia kwa madhumuni ya kiraia, haswa kwa nishati.
Abbas Araghchi amebaini kwamba yake inapanga kujenga vinu vipya 19, kulingana na maandishi ya hotuba ambayo alipaswa kutoa kwenye mkutano na kuchapishwa siku ya Jumanne kwenye ukurasa wake rasmi wa X.
Mnamo mwaka 2018, Bw. Trump aliondoa nchi yake kwenye makubaliano ya nyuklia ya Vienna ya 2015 na kurudisha vikwazo. Katika kulipiza kisasi, Iran ilijitenga hatua kwa hatua na mkataba huo, haswa kwa kurutubisha uranium hadi kiwango cha juu.
Bwana Araghchi alielezea “matumaini ya tahadhari” ya nchi yake wiki hii kuhusu mchakato unaoendelea.
Tangu arejee katika Ikulu ya White House, Donald Trump amezindua upya sera yake inayoitwa “shinikizo la juu” dhidi ya Iran, akiitaka mwezi Machi kujadili makubaliano mapya huku akitishia kuishambulia nchi hiyo ikiwa diplomasia itafeli.
Katika taarifa zilizochapishwa siku ya Ijumaa na Jarida la Time, alihakikisha kwamba yuko tayari kukutana na kiongozi mkuu wa Iran au rais wa nchi hiyo.
Washington ilitangaza vikwazo vipya vinavyolenga sekta ya mafuta ya Iran siku ya Jumanne. Tehran ilishutumu “mbinu ya uadui.”
Waziri wa Iran amesema Alhamisi kwamba yuko tayari kusafiri hadi Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, nchi zingine ambazo ni sehemu ya makubaliano ya Vienna, kwa majadiliano juu ya suala hili.
Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alitoa wito kwa nchi za Ulaya kuamua haraka iwapo watarejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.