
Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amefanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Algeria na pande mbili zimetilia mkazo udharura wa kushirikiana mabunge ya nchi zao kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza na Lebanon.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Ebrahim Azizi, Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ambaye ameongoza ujumbe wa ngazi za juu wa Bunge la Iran katika ziara yake nchini Algeria, ameonana na Spika wa Bunge la nchi hiyo, Ibrahim Boughali na kutilia mkazo wajibu wa kushirikiana nchi za Kiislamu pamoja na mataifa huru kuhakikisha utawala wa Kizayuni unakomesha jinai zake huko Ghaza na Lebanon.
Ebrahim Azizi pia amesema, iwapo hivi sasa hakutachukuliwa hatua za kuomeshwa jinai za utawala wa Kizayuni, basi tuelewe kuwa, Israel haitoishia hapo, bali nchi zote za Ulimwengu wa Kiislamu zitakuwa hatarini.
Amesema, Operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa iliyoongozwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina tarehe 7 Oktoba 2023 ilithibitisha kuwa Israel ni utawala dhaifu na pandikizi, hivyo nchi za Waislamu zinapaswa kuungana katika kuzuia kuendelea jinai za Israel dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Lebanon na Palestina wakiwemo wa Ukanda wa Ghaza.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Algeria amesema kwenye mazungumzo hayo kwamba, nchi yake itaendelea kuwa muungaji mkono wa taifa la Palestina na kwamba uungaji mkono huo wa Algiers kwa kadhia ya Palestina utaendelea kwenye Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa.