Iran imelaani vikali mauaji ya msemaji wa Hizbullah Mohammad Afif katika shambulio la Israel lililolenga jengo moja katikati mwa Beirut, na kusema Shahidi Afif alikkuwa ‘sauti nzito,” ya taifa la Lebanon.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei amemuenzi Shahidi Afif na kumtaja kuwa mtu mashuhuri aliyekuwa na jukumu kuelimisha umma kuhusu dhulma na ukiukwaji unaofanya wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ni utawala ghasibu na wa kibaguzi.
Amesisitiza hadi dakika ya mwisho ya maisha yake kupaza sauti ya ukandamizaji wa watu wa Lebanon na Palestina unaofanywa na utawala wa Israel kote duniani.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amebainisha pia kuwa zaidi ya waandishi wa habari 200 na wafanyakazi wa vyombo vya habari wameuawa shahidi mikononi mwa wanajeshi wa Israel katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, na kuyataja mauaji hayo kuwa ni sehemu ya kampeni iliyoratibiwa na utawala huo wa Kizayuni ya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.
Baghai amesema mauaji haya yanalenga kuvitisha vyombo vya habari, na kuvishinikiza kuacha kuripoti jinai za ukatili wa utawala wa Israel.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa sheria ya kimataifa ya kibinadamu hususan Mikataba ya Geneva ya mwaka 1949 inakataza mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari na wanataaluma wa habari na kulaani mauaji ya Afif na waandishi wengine wa habari huko Lebanon na Gaza kuwa ni mfano wa wazi wa uhalifu wa kivita.

Baghaei aliutaka Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuwawajibisha maafisa wa Israel kwa kufanya ukatili huo.
Alitoa hakikisho kwamba damu ya Afif, kama ile ya mwandishi mashuhuri wa Al Jazeera Shireen Abu Akleh pamoja na wafanyakazi wengine wa vyombo vya habari wa Lebanon na Palestina waliouawa shahidi, itazidi kuipotezea Israel na washirika wake, na itaimarisha azma ya mapambano ya Walebanon na Wapalestina kuendelea na mapamabano halali dhidi ya ubaguzi wa rangi uvamizi wa Israel.
Afif alikuwa mshauri wa muda mrefu wa vyombo vya habari wa marehemu Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyed Hassan Nasrallah, ambaye aliuawa katika shambulio la anga la Israel Septemba 27.
Alisimamia kituo cha televisheni cha al-Manar chenye uhusiano na Hizbullah kwa miaka kadhaa kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa vyombo vya habari katika harakati ya Hizbullah.