Iran imesema mashitaka ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) dhidi ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wake wa zamani wa vita Yoav Gallant pia yalipaswa kujumuisha “mauaji ya kimbari” ya utawala huo ghasibu.
Mahakama ya ICC mnamo Alhamisi kilitoa vibali vya kukamatwa Netanyahu na Gallant kwa mashtaka ya “uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita uliofanywa kuanzia Oktoba 8 2023 hadi 20 Mei 2024“.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei ameandika katika ukurasa wake wa X kwamba: “Baada ya miezi 14 ya kampeni ya mauaji ya kimbari ya utawala ghasibu wa Israel huko Gaza, ambayo ilikuwa na ukatili mbaya zaidi, Mahakama ya Utangulizi ya ICC hatimaye imetoa hati ya kukamatwa kwa wahalifu wawili wakuu Netanyahu na Gallant.”
Ameongeza kuwa: “Bila shaka, mashtaka yao yalipaswa kujumuisha ‘mauaji ya kimbari’ ambayo yako wazi.”
Baghaei amesema, “Tunakaribisha hatua yoyote ya uadilifu na kukomesha hali ya kutoadhibiwa kwa utawala wa Israel kwa mauaji ya kimbari, jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu zinazofanywa katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kwingineko“.
Hali kadhalika Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: “Kuahirisha mambo kwa muda mrefu katika kuiwajibisha Israel – hasa kutokana na vikwazo vya siri na vya wazi vya Marekani na utumiaji mabavu- kumeruhusu uhalifu wa kinyama kuendelea katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu.”
Baghaei amesema “utekelezaji kamili na wa haraka wa hati hizi za kukamatwa utakuwa kipimo cha utendaji kazi wa mfumo wa sheria katika uga wa kimataifa dhidi ya jinai”, akionya dhidi ya ucheleweshaji wowote.

Majaji wa ICC walisema Alhamisi iliyopita kwamba kulikuwa na “sababu nzuri” za kuamini kuwa Netanyahu na Gallant “kwa makusudi na kwa kujua waliwanyima raia katika Gaza vitu ambavyo ni muhimu kwa maisha yao“.
Mahakama hiyo pia ilisema wawili hao wanawajibika kuhusu uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika mashambulizi ya umwagaji damu huko Gaza.
Ikiungwa mkono na Marekani na washirika wake wa Magharibi, Israel ilianzisha vita dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba 2023, baada ya harakati ya muqawama wa Palestina Hamas kutekeleza Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya utawala wa Israel ili kukabiliana na ukatili wa utawala huo dhidi ya Wapalestina.
Mashambulizi ya umwagaji damu ya utawala huo kwenye Gaza hadi sasa yamesababisha vifo vya Wapalestina 44,056 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kujeruhi wengine 104,268. Maelfu zaidi pia wametoweka na inakisiwa kuwa wamekufa chini ya vifusi.