Iran: Mapigo tutakayojibu dhidi ya shambulio la Israel yataendana na sheria za kimataifa

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Jamhuri ya Kiislamu inabaki nayo haki yake ya msingi ya kujibu mashambulio ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya ardhi yake na kwamba ulipizaji kisasi utakaofanywa na Tehran utaendana kikamilifu na sheria za kimataifa.

Amir Saeid Iravani aliyasema hayo jana Jumatatu alipozungumza katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa kwa ombi la Iran la kutaka kujadiliwa mashambulizi yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya maeneo yake ya kiulinzi katika Mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam, ambayo yaliweza kuzimwa kwa mafanikio na vikosi vya Ulinzi wa Anga.

“Kama nchi yenye mamlaka kamili ya kujitawala, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inabaki nayo haki yake ya msingi ya kutoa jibu kwa wakati itakaochagua kwa kitendo hiki cha uchokozi, haki ambayo imethibitishwa wazi chini ya kifungu cha 51 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa”, ameeleza Balozi Iravani akitilia mkazo ahadi iliyotolewa na viongozi mbalimbali wa Iran ya kulipiza kisasi dhidi ya uchokozi uliofanywa na utawala wa Kizayuni.

Aidha, Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amelaani uchokozi wa Israel akiuelezea kuwa ni “ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa” ambao umepelekea kuuawa shahidi wanajeshi wanne wa Iran na raia mmoja.

Askari waliouawa shahidi katika shambulio la Israel

Iravani amebainisha kuwa uchokozi huo uliofanywa na Israel ni sehemu ya mwenendo mpana na endelevu wa uchokozi unaofanywa na utawala huo ghasibu ili kuvuruga eneo lote la Asia Magharibi bila ya kuchukuliwa hatua yoyote ya kuadhibiwa.

Ametaja vita vya mauaji ya kimbari ulivyoanzisha utawala wa Kizayuni Oktoba 2023 dhidi ya Ukanda wa Ghaza na kushadidisha mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya Lebanon kama mifano mikuu ya uchokozi huo.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameeleza kusikitishwa na jinsi Marekani inavyouunga mkono utawala wa Kizayuni bila ya mpaka wala masharti yoyote na kuukingia kifua kwa kukwamisha juhudi zinazofanywa na Baraza la Usalama ili kuuwajibisha utawala huo.

Iravani, amelaani pia misimamo ya madola yanayouhami utawala haramu wa Israel kwa kuunga mkono ukatili na uchokozi wake kwa kuuelezea kama hatua ya “kujilinda,” kisha “bila aibu” kuitaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ijizuie kuchukua hatua…/