Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, madai kwamba Iran ilihusika katika jaribio la kuwaua viongozi wa zamani au wa sasa wa Marekani yanakanushwa vikali na hayana msingi wowote.
Ismail Baqaei Hamaneh ameashiria kuzushwa tuhuma kama hizo huko nyuma, ambazo zilikanushwa vikali na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na zikaja kuthibitika kuwa ni uwongo, na akasema kukaririwa dai hili katika wakati huu ni njama yenye kuchukiza iliyozushwa na duru za Kizayuni na zinazoipiga vita Iran ili kuzidi kutatiza masuala yaliyopo kati ya Marekani na Iran.
Baqai Hamane amesisitiza kuwa, kama ilivyoelezwa hapo awali, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatumia njia zote halali na za kisheria katika ngazi ya ndani na kimataifa ili kuhakikisha haki za wananchi wa Iran zinapatikana.
Ijumaa iliyopita, shirika la habari la Marekani la Associated Press lilisema, limenukuu madai hayo dhidi ya Iran yakitolewa na wizara ya sheria ya Marekanina kuandika kwamba shtaka la jinai limewasilishwa katika Mahakama ya Shirikisho ya Manhattan, ambayo likidai kwamba “afisa mmoja asiyejulikana katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu mnamo Septemba iliyopita alimuomba mtu mmoja aandae mpango wa kumfuatilia na hatimaye kumuua Trump”.

Hiki kinachodaiwa kama ‘njama’ kimeibuliwa siku chache tu baada ya mgombea urais wa chama cha Democratic Kamala Harris kushindwa na Donald Trump wa Republican katika uchaguzi wa rais wa Marekani.
Katika mwendelezo wa igizo la kueneza hofu na chuki dhidi ya Iran, maafisa wa serikali ya shirikisho ya Marekani wameshadai mara kadhaa kwamba “Iran inaendelea kufanya njama za kuwaua maafisa wa serikali, ikiwa ni pamoja na Trump, ndani ya ardhi ya Marekani”.
Katika msimu wa joto uliopita, wizara ya sheria ya Marekani ilidai kuwa mwanamume mmoja Mpakistan anatuhumiwa kuwa na uhusiano na Iran katika mpango wa kukodiwa kwa kulipwa fedha ili kufanya mauaji…/