Iran kuweka sentrifuji za kisasa kujibu hatua ya Bodi ya Magavana ya IAEA kupitisha azimio dhidi yake

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran ametoa amri ya kuchukuliwa hatua madhubuti ikiwa ni pamoja na kuwekwa majimui maalumu ya mashinepewa (centrifuges) mpya na za kisasa za aina tofauti kufuatia azimio lisilo na sababu lililopitishwa na Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA dhidi ya mpango wa amani wa nyuklia wa Iran.

Wizara ya Mambo ya Nje na Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran zimetoa taarifa maalumu kuhusu azimio lisilo na uhalali lililotolewa na Bodi ya Magavana ya IAEA kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran ikieleza kwamba: katika kikao cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki mnamo Novemba 21, kwa shinikizo na ung’ang’anizi wa nchi tatu za Ulaya na Marekani, na licha ya kutoungwa mkono na karibu nusu ya nchi wanachama, limepitishwa azimio lisilo la kauli moja kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran.

Taarifa hiyo imeongezea kwa kusema: sera ya msingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ni ya kuwa na maelewano yenye kujenga na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ndani ya fremu ya haki na wajibu ulioainishwa chini ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji (Silaha za Nyuklia) na makubaliano ya usimamizi kamili, na kuhusiana na hili viongozi wa Iran wamekaribisha ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki mjini Tehran ili kuandaa mazingira mwafaka ya kuimarishwa maelewano baina ya Iran na IAEA.

Wizara ya Mambo ya Nje na Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran zimeongezea kusema katika taarifa yao: “kwa msingi huu, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran ametoa amri ya kuchukuliwa hatua madhubuti za kuwekwa majimui maalumu ya mashinepewa (centrifuges) mpya na za kisasa za aina tofauti.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesema: ni wazi kwamba, hatua hizo zinatekelezwa kwa lengo la kulinda maslahi ya Iran na kustawisha zaidi kadiri iwezekanavyo sekta ya nyuklia yenye malengo ya amani, kwa mujibu wa mahitaji ya kitaifa yanayozidi kuongezeka na ndani ya fremu ya haki na majukumu ya Iran kwa mujibu wa makubaliano kamili ya usimamizi; na wakati huohuo ushirikiano wa kiufundi na kiusimamizi na IAEA utaendelea kama ilivyokuwa awali na kulingana na hati ya makubaliao ya usimamizi…/