Iran kutumia diplomasia amilifu kukabiliana na vitisho vya utawala wa Kizayuni

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, diplomasia amilifu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko uwanjani kwa lengo la kunufaika na suhula na uwezo wote uliopo kwa ajili ya kukabiliana na vitisho hatari vya utawala ghasibu wa Israel.

Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika ujumbe alioutoa kwenye akaunti yake binafsi ya mtandao wa kijamii wa Instagram, kuwa katika mkutano na waandishi wa habari akiwa na waziri mwenzake wa Iraq hivi karibuni, amesisitiza haja ya kuchukuliwa hatua za haraka kwa madhumuni ya kukomesha jinai za kivita zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya watu wa Palestina na Lebanon.

Katika safari zake katika siku chache zilizopita katika nchi za Lebanon, Syria, Saudi Arabia, Qatar na Iraq, Abbas Araghchi ametoa ujumbe wa wazi kwa eneo na dunia nzima, ambapo amefanya mashauriano muhimu ya kidiplomasia kuhusu suala hilo. Katika mazungumzo na viongozi wa nchi hizo amesisitiza haja ya kukomeshwa mara moja jinai za utawala wa Kizayuni, na utayari wa Iran wa kutumia sambamba njia zote mbili za amani na vita ili kufikia lengo hilo.

Akiwa mjini Baghdad, Araghchi alikutana na kuzungumza na Rais Abdul Latif Jamal Rashid, Waziri Mkuu Mohammad Shia al-Sudani na Fuad Hussein, Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Iraq.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ameelekea Muscat, mji mkuu wa Oman, leo Jumatatu asubuhi ikiwa ni katika sehemu ya safari zake za kieneo kwa ajili ya kufanya mashauriano ya kidiplomasia kwa lengo la kusimamisha jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya raia wasio na hatia wa mataifa ya eneo hili.

Mara tu baada ya kuwasili Muscat, Araghchi amekutana na kuzungumza na Sayyid Badr Al-Busaidi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Usultani wa Oman.