Mohammad Reza Aref, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema kuwa kufanyika kura ya maoni inayohusisha Wapalestina wote ndilo suluhisho pekee, la kudumu na la kidemokrasia kwa suala la Wapalestina.
Aref ametoa kauli hiyo katika hotuba yake kwenye Kikao cha Dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh. Amesema Iran inapendekeza kura ya maoni yenye kushirikisha Wapalestina wote, ikiwa ni pamoja na Waislamu, Wakristo na Wayahudi kwa msingi wa kanuni ya “kila Mpalestina, kura moja.” Ameongeza kuwa pendekezo hilo litarejesha haki ya Wapalestina na kuwawezesha kuamua hatma yao.
Aref aidha amesema, Iran pia inaamini kuwa kuepuka mgawanyiko kati ya nchi za Kiislamu ni mkakati wa kukabiliana na njama za wale wanaowatakia mabaya Waislamu.
Makamu wa Rais wa Iran ameukosoa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kukiuka bila aibu kanuni na sheria zote za kimataifa, kurarua Hati ya Umoja wa Mataifa katika Baraza Kuu na kumpiga marufuku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuingia katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Aref amesema kuna “janga la aibu” katika uhalifu wa Israel huko Palestina kwa zaidi ya mwaka mmoja na nchini Lebanon katika kipindi cha mwezi uliopita. Amesema jinai za Israel zina mizizi katika “kukosa kuadhibiwa wahalifu” ambapo wanatenda jinai kwa sababu wana yakini kuhusu “msaada usio na shaka” wa Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi.
Zaidi ya viongozi 50 wa nchi za Kiarabu na Kiislamu wameshiriki kwenye mkutano huo wa dharura wa mjini Riyadh ambao umeitishwa kufuatia pendekezo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Akiwa mjini Riyadh, Mohammad Reza Aref, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amekutana na kufanya mazungumzo na Mwanamfalme Mohammad Bin Salman Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia. Aref ameyataja mazungumzo yake na Bin Salman kuwa mazuri sana na kusema nchi hizi mbili jirani zinaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuleta amani na utulivu wa kieneo.