Iran: Dunia isimame kutetea wanawake wa Kipalestina

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametuma ujumbe katika mtandao wa kijamii wa X kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kupigwa Marufuku Ukatili dhidi ya Wanawake ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Novemba, akizungumzia jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wanawake na wasichana wa Palestina hasa katika Ukanda wa Gaza.

Ismail Beqaei ameandika kwenye akaunti yake binafsi katika mtandao wa X kwamba: Katika Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Ukatili dhidi ya Wanawake, tukumbuke ukatili mkubwa wa miongo kadhaa ya uvamizi wa kikatili na mauaji ya kimbari ya kikoloni katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameongeza kuwa: “Kiwango na ukubwa wa ukatili dhidi ya wanawake na wasichana wa Gaza ni jambo lisilo na kifani na la kushtua. Katika mwaka mmoja uliopita makumi ya maelfu ya wanawake na wasichana wa Kipalestina wameuawa au kujeruhiwa, na akina mama wote, wanawake na wasichana huko Gaza, wako katika hatari ya njaa na kulazimishwa kuhama makazi yao mara kwa mara.

Baqaei amesema: Ulimwengu lazima usimame kuwatetea wanawake na wasichana wa Kipalestina.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya ya Palestina, idadi ya mashahidi wa Kipalestina waliouawa na Israel tangu kuanza mauaji ya kimbari ya utawala huo huko Gaza imefikia watu 44,211, zaidi ya 70% kati yao wakiwa wanawake na watoto.