IPTL yakwaa kisiki kesi ya kuidai Serikali mabilioni

Dar es Salaam. Kampuni ya kufua umeme wa mafuta, Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imekwama kwenye kesi iliyotaka kufungua dhidi ya Serikali baada ya Mahakama Kuu kuikataa.

Kampuni hiyo ilifungua kesi ya madai dhidi ya Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, ikipinga mkataba wa makubaliano ya kumaliza kesi ya madai iliyofunguliwa na Serikali dhidi yake.

Serikali katika kesi hiyo ya madai ilikuwa ikiidai IPTL pamoja na mambo mengine kurejesha zaidi ya Dola za Marekani 198.879 milioni (zaidi ya Sh536.5 bilioni kwa sasa) ilizojipatia kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow.

Mkataba wa makubaliano ya kumaliza kesi hiyo ulisainiwa na pande zote Machi Mosi, 2021.

Kesi hiyo ilimalizika kwa njia ya maridhiano kufuatia mkataba wa makubaliano iliyosainiwa na pande zote Machi Mosi, 2021 na Mahakama ikatoa uamuzi wa kumalizika kwake, Machi 19, 2021.

Hata hivyo, miaka mitatu baadaye, 2024 IPTL iliigeuka Serikali baada ya kufungulia kesi. Katika kesi hiyo ya madai ya mwaka 2024 IPTL iliupinga mkataba huo wa makubaliano ya kumaliza kesi hiyo ikidai kuwa ni batili.

Pamoja na mambo mengine, IPTL, ilidai kuwa mwenyekiti na mkurugenzi mtendaji wake (Sethi) alilazimishwa kusaini makubaliano hayo yanayoilazimisha kulipa Dola za Marekani 148.4 milioni za tuzo Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID), kwenye shauri ambalo haikuwa mdaawa.

Hivyo pamoja nafuu nyinginezo iliomba Mahakama itengue makubaliano hayo na iamuru ilipwe fidia ya usumbufu Sh100 bilioni.

Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa Mei 16, 2025 na Jaji Awamu Mbagwa baada ya kuchambua ushahidi na hoja za pande zote imeikatalia IPTL na kuridhika kuwa makubaliano hayo ni halali.

“Kwa mujibu wa yaliyoelezwa hapo juu, kuwa mdai ameshindwa kuthibitisha madai yake kwa mizania ya uwezekano, ninatupilia mbali shauri hili kwa sababu halina mashiko ya kisheria. Wadaiwa wanastahili kulipwa gharama za shauri hili,” amesema Jaji Mbagwa akihitimisha hukumu hiyo.

Kesi hiyo ilitokana na mchakato wa uhamishwaji wa pesa zilizokuwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu (BoT) kwenda IPTL.

Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa pamoja na Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na IPTL kutokana na mgogoro wa mkataba wa umeme hasa kuhusu bei ya umeme.

Hivyo pande zote zilikubaliana kuweka katika akaunti hiyo pesa ambazo ilipaswa kuilipa IPTL, ili kusubiri kumalizika kwa mgogoro huo, katika Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID).

Septemba 5, 2013, Mahakama Kuu Dar es Salaam ilitoa amri ya kuimilikisha IPTL kwa Sethi, kupitia kampuni yake ya Pan Africa Power Solutions (T) Limited (PAP).

Sethi alidai kampuni zake hizo zilikuwa zimenunua hisa za wabia wa IPTL, kwamba PAP ilinunua hisa za VIP Engineering and Marketing ya mfanyabiashara James Rugemalira (asilimia 30).

Pia alidai kuwa kampuni yake ya Piper Link ilinunua hisa za Mechmar Corporation (Malaysia) Berhad (asilimia 70) na kisha Piper Link ikaiuzia PAP.

Hivyo Oktoba 21, 2013, IPTL chini ya  PAP / Sethi, mwenyekiti na mkurugenzi mtendaji mpya wa IPTL,  iliingia mkataba na  Serikali  unaoitwa: “Mkataba wa Uwasilishaji wa Fedha kwa Independent Power Tanzania Limited.”

Mkataba huo ulimuagiza na kumwelekeza Wakala wa Escrow (BoT) kuhamisha na kuwasilisha kwa IPTL fedha zote zilizohifadhiwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.

Ili kuilinda Serikali, Oktoba 27, 2013, pande hizo ziliingia mkataba mwingine uitwao “Hati ya Ulinzi”, iliyosainiwa na Sethi, mwenyekiti na mkurugenzi mtendaji wa IPTL.

Katika hati hiyo IPTL alikubali kwa hiari kuilinda Serikali na Wakala wa Escrow dhidi ya madai yote ya baadaye, mashauri na hatua za kisheria zitakazojitokeza kutokana na kuhamishwa  kwa fedha kwenda kwake, kwa mujibu wa Mkataba wa Uwasilishaji wa Fedha.

Hivyo fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow zililipwa kwa IPTL.

Hata hivyo, wakati huo IPTL ilikuwa chini ya usimamizi wa Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK), iliyokuwa ikiidai deni la mkopo wa uwekezaji.

Hivyo SCB-HK iliishtaki Serikali ya Tanzania ICSID, ikidai fedha hizo na ICSID, iliiamuru kuilipa SCB-HK Dola za Marekani 198,879,972.70.

Kufuatia Tuzo ya Usuluhishi ya ICSID, ndipo Serikali ya Tanzania, kupitia AG na Katibu Mkuu Nishati, ikaishtaki IPTL, kwa mujibu wa Mkataba wa Ulinzi baina ya pande hizo, ikiitaka irejeshe fedha hizo ilizoamiriwa na ICSID kuilipa SCB-HK.

Wakati kesi hiyo inaendelea, pande zote zilianza mazungumzo kumaliza kesi hiyo kwa makubaliano.

Sethi ambaye alikuwa mahabusu kwa kesi ya uhujumu uchumi iliyotokana na uchotwaji wa pesa hizo za Escrow, aliwakilishwa na Manjit Singh Sethi aliyempa mamlaka ya uwakilishi huo na Wakili Omar kusimamia kesi hiyo na kushiriki majadiliano hayo.

Hatimaye pande zilifikia makubaliano yaliyohitimisha kesi hiyo ya Serikali, ambaye kwa upande wa IPTL yalisainiwa na Sethi mwenyewe, kabla ya kugeuka na kufungua kesi hii ya kuyapinga.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, Sethi katika ushahidi wake pamoja na mambo mengine alidai kuwa Machi Mosi, 2021, alipokuwa rumande katika Gereza la Ukonga, aliitwa katika chumba maalumu.

Chumbani humo aliwakuta Profesa Adelardus Kilangi, Mwanasheria Mkuu wa wakati huo, Biswalo Mganga, Mkurugenzi wa Mashtaka wa wakati huo, na watu wengine wawili wenye silaha.

Hivyo, alilazimishwa kusaini mkataba wa makubaliano hayo.

Jaji Mbagwa katika hukumu hiyo baada ya kuchambua ushahidi na vielelezo mbalimbali vya nyaraka kwa pande zote amesema kuwa ushahidi unathibitisha kuwa Sethi alikuwa tayari kumaliza kesi hiyo kwa makubaliano hata kabla ya tarehe ya kusaini makubaliano hayo.

“Kutokana na hayo, hoja kwamba alilazimishwa kusaini makubaliano ya suluhu Machi Mosi, 2021 ni ya kubuni na haina mashiko”, amesema Jaji Mbagwa.

Kuhusu madai kuwa mawakili Omar Omar na Alex Balomi hawakuteuliwa katika iliyofunguliwa na Serikali na  kutokumuidhinisha Manjit kushiriki katika majadiliano, Jaji Mbagwa amesema anashangaa mdai kutokuwahusisha katika kesi hiyo wala kuwaita kuwa mashahidi wake waeleze walipata wapi mamlaka hayo.

“Kwa mtazamo wangu Kutowashirikisha watu hao watatu, ilikuwa ni mbinu ya kukwepa ushahidi ambao ungeondoa madai ya mdai”, amesema na kusisitiza:

“Kwa kuzingatia maelezo hayo hapo juu, ninahitimisha kuwa mkataba wa makubaliano  ni halali kwa kuwa ulisainiwa kwa hiari na ridhaa kamili ya pande zote mbili na unazifunga pande zote kulingana na Kifungu cha 10 cha Sheria ya Mikataba.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *