Inter Milan jana ilionyesha ukomavu kwa kufunga mabao mawili ikiwa imetoka nyuma baada ya kutanguliwa na Barcelona katika mechi ya pili ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuibuka na ushindi wa mabao 4-3 nyumbani kwenye Uwanja wa San Siro Italia na kutinga hatua ya fainali ya mashindano hayo.
Matokeo hayo yameifanya Inter kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-6 kutokana na mechi ya kwanza baina yao ambayo Barcelona ilikuwa nyumbani wiki iliyopita kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.

Inter ilitangulia kupata bao la kuongoza kupitia kwa Lautaro Martinez aliyefunga katika dakika ya 21 akimalizia pasi ya Denzel Dumfries na dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza, Hakan Calhanoglu akaifungia bao la pili kwa mkwaju wa Penalti.
Penalti hiyo ilitolewa na refa Syzmon Marciniak baada ya Lautaro Martinez kuangushwa ndani ya eneo la hatari la Barcelona.
Upepo wa mechi ulibadilika katika kipindi cha pili ambacho Barcelona walilishambulia kama nyuki lango la Inter Milan na kupata mabao hayo matatu ambayo yamewavusha kwenda fainali ya mashindano hayo msimu huu.
Dakika ya 54, Eric Garcia alitumia vyema pasi ya Gerard Martin kuipatia Barcelona bao la kwanza kisha baadaye dakika ya 60, Barca ikapata bao la kusawazisha kupitia kwa Dani Olmo aliyemalizia kwa kichwa krosi ya Gerard Martin.
Ilionekana kama Barcelona imeshamaliza mechi baada ya kupata bao la tatu kupitia kwa Raphinha katika dakika ya 88 lakini katika dakika za majeruhi Francesco Acerbi akaisawazishia Inter akimalizia pasi ya Dumfries.
Matokeo hayo yalidumu hadi refa Marciniak alipopuliza kipyenga cha kuashiria kumalizika kwa dakika 90 na hivyo kulazimisha mchezo huo kwenda katika dakika 30 za nyongeza.
Ushindi kwa Inter Milan ulipatikana katika dakika ya 99 kupitia bao la Davide Frattesi aliyetumia vyema pasi ya Mehdi Taremi kuipatia timu yake bao la nne kwa shuti la mguu wa kulia.
Baada ya bao hilo, Inter Milan walionekana kuwa imara katika safu yao ya ulinzi ambayo ilifanikiwa kujilinda vyema hadi refa Marciniak alipopuliza filimbi ya kumaliza mchezo.
Huo ni ushindi wa tatu kwa Inter Milan katika mechi 14 ilizokutana na Barcelona ambapo imepoteza mechi sita na zimetoka sare mara tano.
Hiyo ni mara ya pili kwa Inter Milan kutinga hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ndani ya misimu mitatu ya hivi karibuni.
Imekuwa ni mara ya nane kwa Barcelona kutolewa katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya jambo linaloifanya iongoze sawa na Real Madrid.

Inter Milan sasa inasubiria mshindi baina ya PSG zinazocheza leo ambaye itakabiliana naye katika mechi ya fainali itakayochezwa kwenye Uwanja wa Allianz Arena Ujerumani, Mei 31, mwaka huu