Injinia Hersi asimamisha Bunge, Kigogo Simba, Karia washangiliwa

Ukumbi wa Bunge leo uligubikwa kwa kelele za shangwe na makofi ya kugonga meza wakati wa utambulisho wa viongozi wa mpira wa miguu nchini Tanzania walioongozwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Wallace Karia.

Utambulisho wa viongozi hao ulivutia hisia na kuonyesha ushabiki mkubwa wa wabunge kwa timu za Simba na Yanga ingawa kwenye masikio ya kawaida, waliomshangilia Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said walikuwa wengi zaidi.

Kiongozi mwingine wa soka aliyetambulishwa mbali ya Karia na Hersi, ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba, Seleman Said.

Utambulisho wa viongozi hao ulianzia kwa Karia, akafuata Injinia Hersi kabla ya kumalizia na Seleman Said, lakini shangwe zaidi lililipuka kwa mgeni wa pili huku sauti zikisikika kutoka kwa wabunge kuwa ‘hatuchezii’.

Rais wa TFF, Walace Karia

Aidha, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu amemuomba Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi atoe mwaliko kwa viongozi wa timu mbili kubwa nchini ambao ni Mohamed Dewji (Simba) na Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ wa Yanga.

“Mheshimiwa Waziri wakati mwingine tunaomba uwaalike viongozi wakuu wa klabu za Simba na Yanga ambao ni Mo Dewji na Ghalib Said ili waje hapa bungeni, tunajua klabu hizi zinaleta maendeleo makubwa,” amesema Naibu Spika, Zungu.

Mbunge wa viti maalum, Ester Bulaya ambaye ni shabiki wa Yanga akipiga makofi

Amesema klabu hizo mbili zinaheshimika, viongozi wao wanaheshimika, wanachama wanaheshimika na zinasaidia kuwaweka Watanzania pamoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *