INEC mguu sawa kugawa majimbo, wadau waonyesha njia

Moro/Dar.  Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuanza mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi , hatua ambayo imewaibua wadau wakionyesha njia sahihi ya kufikia lengo hilo.

Katika maandalizi hayo, Inec imesema itaanza kupokea mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali kuanzia kesho Februari 27 hadi Machi 26, mwaka huu.

Kwa sasa, Tanzania ina jumla ya majimbo ya uchaguzi 264, Tanzania Bara yakiwa 214 na Zanzibar 50.

Akizungumza leo Jumatano Februari 26, 2025 mjini Morogoro baada ya kumaliza kikao kazi cha INEC, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Jacobs Mwambegele amesema:

“Kwa kuzingatia masharti ya kanuni ya 18(1) ya kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za mwaka 2024, napenda kutoa taarifa kwa umma kwamba, kuanzia kesho siku ya Alhamisi tarehe 27 Februari, 2025 Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi itaanza mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi hadi Machi 26, 2025.”

Jaji Mwambegele amesema Tume inatekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa ibara ya 74 (6) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kifungu cha 10(1)(d) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024, ambavyo vimeipa Tume jukumu la kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge.

Amesema kwa mujibu wa ibara ya 75(4) ya Katiba, jukumu hilo linaweza kufanywa na Tume mara kwa mara na angalau kila baada ya miaka 10.

“Kwa kuzingatia masharti hayo ya Katiba, kwa mara ya mwisho Tume ilichunguza mipaka na kugawa majimbo ya uchaguzi katika Jamhuri ya Muungano mwaka 2015, ambapo majimbo mapya 26 yalianzishwa,” amesema akisisitiza mapendekezo yafuate masharti.

Tamko hilo la Tume limekuja kipindi ambapo kuna mjadala kuhusu namna mgawanyo wa majimbo hapa nchini usivyo na uwiano sawa kati baadhi ya maeneo na mengine.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu aliibua suala hilo alipozungumza jijini Dar es Salaam, alitolea mfano idadi ya watu katika majimbo ya Zanzibar na majimbo Tanzania Bara; pamoja na majimbo ya mijini na yale ya vijijini.

Lissu alisema badala ya kuangalia idadi ya watu kupata uwakilishi sahihi ambao ndio msingi wa mgawanyo, tume imekuwa inaangalia jiografia yaani ukubwa wa eneo, milima na mabonde.

Mtazamo wa Lissu unaungwa mkono na Profesa Mohammed Makame kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) ambaye amesema kama ugawaji wa majimbo utazingatia idadi ya watu na si ukubwa wa eneo litakuwa jambo jema.

Licha ya kuwapo kwa tetesi kwamba baadhi ya majimbo kama Kawe, Mbeya Mjini na mengine, yanatajwa kuwa makubwa na watu wanatamani yagawanywe, Profesa makame amesema si jambo baya kama yatakuwa yamekidhi vigezo vya sheria.

“Yanapogawanywa yagawanywe kutegemeana na idadi ya watu na si kwa kuangalia mipaka ya ukubwa wa eneo,” amesema.

Profesa huyo amesema jimbo linaweza kuwa na ukubwa wa eneo, lakini likakosa uwakilishi mzuri wa watu, hivyo katika mchakato huo kinachotakiwa kuzingatiwa ni idadi ya watu si ukubwa wa eneo.

Hata hivyo, Profesa Makame amesema mchakato huo ulitakiwa ufanyike mapema ili kutoa fursa kwa wananchi na wadau kushiriki kikamilifu kutoa maoni yao.

“INEC imefanya hivi ni hatua moja ya ushirikishwaji wa wananchi, kikubwa ni kuangalia majimbo na vituo pia,” amesema.

Amesema ushirikishwaji huo unaipa tume fursa ya kupata maoni ya kina, mtazamo na fikra za wananchi kuhusu majimbo yao ya uchaguzi.

Licha ya kuunga mkono hatua hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya ameeleza wasiwasi wake kuhusu muda sahihi wa kufanya hivyo.

 “Imebaki miezi sita kabla ya kuingia kwenye uchaguzi unataka kuongeza majimbo, hii si sawa. Muda ni mchache wa kukusanya maoni naweza kusema wamekurupuka, hili jambo linafahamika, na tume siku zote ipo, kwa nini hawakufanya marekebisho haya mapema, wanasubiri mpaka muda umebaki mchache?”

Amesema uamuzi wa Tume ulipaswa kulipatia kipaumbele jambo hilo kwa kuwa ni miongoni mwa mambo ya msingi yanayopaswa kufanyika mapema.

“Walikuwa na miaka minne ya kufanya kila kitu, lakini kinachofanyika ni zimamoto, ingawa wazo ni nzuri tatizo ni muda waliotangaza,” amesema Sakaya aliyewahi kuwa mbunge wa Kaliua mkoani Tabora.

Suala la muda pia limehojiwa pia na Riziki Mngwali, waziri kivuli wa Elimu wa ACT- Wazalendo aliyesema huenda INEC tayari ina uamuzi wake lakini imetumia mwamvuli wa kukusanya maoni kama kivuli cha kuufikia uamuzi huo.

“Nimeshangaa kuiona taarifa hiyo wakati huu, inafahamika kwamba mwaka huu ni wa uchaguzi ilikuwaje hawakuliona hili na wakaanza kukusanya maoni mapema zaidi ili wapate yenye tija. Sioni nia njema hapa wala huo ushiriki wa wananchi kikamilifu, ni wazi wana maamuzi yao,” amesema Mngwali ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho.

Hata hivyo, Katibu wa NLD, Doyo Hassan Doyo yeye alikuwa na mtazamo tofauti, akisema ugawaji huo wa majimbo utakuwa na afya kwa namna mbili.

“Kwanza, utapunguza ukubwa wa majimbo baadhi na pili itasaidia kuwapa wawakilishi wa majimbo ambao ni wabunge fursa ya kuwajibika vema.

“Kuna majimbo mengine ni makubwa mno, kwa hiki inachotaka kukifanya INEC kuyagawa, kitakuwa na afya,” amesema.

Hata Katibu Mkuu wa UDP, Saumu Rashid, amesema kuwa hatua inayochukuliwa na INEC ni sahihi na yenye manufaa, kwani inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na Katiba.

“Tume inaongozwa kwa mujibu wa sheria na inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba, hivyo inatimiza wajibu wake.

“Ni hatua muhimu na yenye manufaa kwa kuweka utaratibu wa kupata mapendekezo kuhusu suala hili.

“UDP itakutana katika vikao vyake na kujadiliana kabla ya kutoa maoni rasmi kuhusu muundo wa ugawaji wa majimbo haya,” amesema Saumu.

Mbali na mitazamo ya wadau hao, Mchambuzi wa habari za Maendeleo ya Kijamii, Bubelwa Kaiza amekosoa msingi wa mgawanyo akisema vigezo vya kikatiba haviko wazi.

“Lazima tujue kama kigezo cha kugawa jimbo ni ukubwa wa eneo au idadi ya watu, lakini jinsi ilivyo sasa, hakuna kigezo kilichosimama, ndiyo maana Tume inajiamulia,” amesema akisisitiza kuwa “Huo ni udhaifu ambao upo kwenye Katiba na unapaswa kufanyiwa kazi kurekebishwa.”

Amesema mabadiliko ya majimbo mara nyingi huchagizwa na Serikali, mathalan, pale wanapoona sehemu fulani wanaweza kushindwa, hutenga jimbo mara mbili.

Vilevile, Kaiza amesema ukubwa wa Bunge umekuwa ukiongezeka kila baada ya muda Fulani, lakini tija ya uwakilishi wa wananchi bado haionekani na wanaendelea kuwa na maisha magumu.

“Lazima Katiba itamke bayana Bunge letu linatakiwa kuwa na wabunge wangapi, wasiongezeke. Kitakachotengwa yawe ni maeneo yote kwa ukubwa sawa, waongezeke watu au wasiongezeke miaka yote itabaki hivyo,” amesema.

Hata hivyo, amesema kwa kuwa jambo hilo linabebwa kisiasa zaidi, ni bora kuachana na majimbo na badala yake kuwepo na uwakilishi wa uwiano.

“Kila chama kipate idadi ya wabunge kulingana na uwiano wa kura walizopata kama wanavyofanya Ujerumani au Afrika Kusini, mkipata asilimia 30 na wabunge mnapata kwa kiwango hicho,” amesema.

Masharti ya mapendekezo

Jaji Mwambegele amewakumbusha wadau wote wenye maombi wahakikishe mapendekezo yao yanajadiliwa katika Kamati ya Ushauri ya Wilaya, kisha yawasilishwe kwa Katibu Tawala wa Mkoa kwa ajili ya kujadiliwa katika Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na Katibu Tawala wa Mkoa awasilishe kwenye Tume mapendekezo yaliyopitishwa na RCC sambamba na viambatisho vyote.

Amesema moja ya vigezo vitakavyotumika ni wastani wa idadi ya watu na kwa majimbo yaliyoko mijini ni kuanzia wastani wa watu 600,000 wakati yale ya vijijini wastani wake ni kuanzia watu 400,000.

Ameongeza kuwa, idadi ya watu itakayotumika ni ile iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

Jaji Mwambegele amevitaja vigezo vingine kuwa ni hali ya kiuchumi ya jimbo, ukubwa wa eneo la jimbo husika, mipaka ya kiutawala, jimbo moja kutokuwa ndani ya wilaya au halmashauri mbili, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, uwezo wa ukumbi wa Bunge, idadi ya wabunge wa viti maalumu wanawake, upatikanaji wa njia za mawasiliano na hali ya kijiografia ya eneo linalokusudiwa kugawanywa.

Pia, amesema halmashauri zinazokusudia kubadili jina la jimbo, nazo zinapaswa kufuata utaratibu kama ule unaotumika katika kuwasilisha maombi ya kugawa majimbo.