Indonesia yaeleza hamu yake ya kuwa mwanachama wa Bunge la Qur’ani la Ulimwengu wa Kiislamu

Mkurugenzi Mkuu wa Miongozo ya Jamii ya Kiislamu wa Wizara ya Dini ya Indonesia ametangaza kuwa nchi yake iko tayari kujiunga na Bunge la Qur’ani la Ulimwengu wa Kiislamu.

Mtandao wa Sahab umelinukuu Shirika la habari la Ahlul-Bayt (as) na kuripoti kuwa, Qamaruddin Amin, ameeleza hayo katika mazungumzo aliyofanya na Hujjatul Islam Seyyed Mustafa Hosseini Neishaburi, Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Qur’ani na Tablighi cha Shirika la Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu la Iran.

Amin ameongeza kuwa Jakarta imeamua kuchukua uamuzi huo baada ya kuchunguza fursa zilizopo za kuongeza mashirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa Qur’ani Tukufu.

Mkurugenzi Mkuu wa Miongozo ya Jamii ya Kiislamu wa Wizara ya Dini ya Indonesia amekaribisha mpango wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuunda Bunge la Qur’ani la Ulimwengu wa Kiislamu na akasema, hilo ni jambo la busara na la lazima, na akatangaza utayarifu wa nchi yake wa kuwa mwanachama wa bunge hilo.

Katika mazungumzo hayo, Hujjatul-Islam Hosseini Neishabouri amesema, leo wanadamu wanavutiwa zaidi kusikia wito wa kufariji nyoyo wa amani, uadilifu na uhuru kuliko ilivyokuwa huko nyuma na akabainisha kwamba: hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuzidi kupanua mawasiliano na mataifa na madola mengine katika uga wa Qur’ani inalenga kufikisha ujumbe wa umoja na mshikamano duniani ambao utaweza kuthibiti chini ya kivuli cha fikra za Qur’ani.

Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Qur’ani na Tablighi cha Shirika la Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: diplomasia ya kujenga umoja ya Qur’ani Tukufu ina maana ya kuratibu mahusiano ndani ya Jamii ya Kiislamu, kuanzia kwenye makundi hadi madhehebu za Kiislamu na vilevile mahusiano kati ya Jamii ya Kiislamu na jamii zisizo za Kiislamu kwa kuzingatia nadharia ya “Umma Mmoja wa Kiislamu”.

Inafaa kuashiria kuwa, Indonesia ndiyo nchi ya Waislamu yenye idadi kubwa zaidi ya watu, na daima imekuwa ikitambulika kuwa ni moja ya mifano maarufu ya kuishi kwa amani na masikilizano wafuasi wa dini na madhehebu mbalimbali…/