
Mamlaka ya India siku ya Jumatano, Aprili 24, imechukua mfululizo wa hatua za kidiplomasia dhidi ya Pakistani, ikiishutumu kwa “ugaidi wa kuvuka mpaka” kufuatia shambulio baya dhidi ya watalii huko Kashmir ambalo lilisababisha vifo vya watu 26.
Imechapishwa:
Dakika 3
Matangazo ya kibiashara
Shambulio hilo lilileta uhusiano kati ya majirani hao wawili wenye silaha za nyuklia katika kiwango chao kibaya zaidi kuwahi kutokea kwa miaka mingi, huku wengine wakihofia kwamba hatua za kidiplomasia za New Delhi ni mwanzo tu katika msururu wa hatua, kukiwa na hatari ya hatua ya kijeshi.
Hatua za India, kama vile kusitisha mkataba wa kugawana maji, kufunga kivuko kikuu cha mpaka wa nchi kavu kati ya nchi hizo mbili na kuwaita wanadiplomasia, zinakuja siku moja baada ya watu wenye silaha kufyatua risasi katika eneo lenye watalii katika eneo linalotawaliwa na India, Kashmir na kuua Wahindi 25 na Mnepali mmoja.
Siku ya Jumatano, Waziri wa Ulinzi wa India alisema kwamba “wale waliohusika na washirika wa kitendo kama hicho watasikia majibu yetu haraka sana,hatutakuwa na huruma.”
Maji chimbuko la mgogoro
Afisa mkuu wa wizara ya mambo ya nje ya India, Vikram Misri, ametangaza kwamba “Mkataba wa Indus Waters wa mwaka 1960 utasitishwa mara moja” hadi “Pakistani itakapokataa kabisa kuunga mkono ugaidi wa kuvuka mpaka.” Mkataba huu kinadharia unagawanya maji kati ya nchi hizo mbili, lakini umezua migogoro mingi. Islamabad kwa muda mrefu imekuwa na hofu kwamba India, ambayo iko juu ya mto, ingezuia upatikanaji wake wa maji.
India imesema imewaagiza washirika wa ulinzi wa Islamabad na maafisa wengine wa jeshi la Pakistani walioko New Delhi kuondoka nchini humo ndani ya wiki moja, na kwamba itawaondoa washauri wake wa ulinzi, wanamaji na jeshi la anga kutoka Pakistan.
“India itawatambua, kuwasaka na kuwaadhibu magaidi wote”
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, ambaye amekatisha ziara yake ya kiserikali nchini Saudi Arabia, alishutumu “kitendo hicho kiovu” na kuahidi kwamba washambuliaji “watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.” Akihutubia umati wa watu huko Bihar siku ya Alhamisi, Aprili 24, Narendra Modi alikuwa makini na alitumia Kiingereza kuhutubia ulimwengu. “Magaidi waliwaua watu wasio na hatia. Waliwalenga maskini zaidi. Kuna mamia ya maelfu ya wenzetu wanaoteseka. Ninauambia ulimwengu wote: “India itawatambua, kuwasaka na kuwaadhibu magaidi wote na washirika wao. Tutawawinda hadi dakakika ya mwisho.”
Wakati huohuo, mivutano inaongezeka nchini India, anaripoti mwandishi wetu huko Bangalore, Côme Bastin. Wanafunzi wengi kutoka Kashmir inayoshikiliwa na India wamekabiliwa na unyanyasaji na vitisho kutoka kwa mamlaka kufuatia shambulio hilo. Makundi kadhaa ya itikadi kali za Kihindu pia yametoa vitisho vya kuuawa dhidi ya Waislamu wa India.
Pakistani kuchukuwa hatu za kulipiza
Siku ya Alhamisi, maafisa wakuu wa kiraia na kijeshi wa Pakistani walikutana kwa saa mbili, na baada ya mkutano huo, ofisi ya Waziri Mkuu Shehbaz Sharif imetangaza hatua kadhaa dhidi ya jirani yake na mpinzani wake wa kihistoria. Msururu huu wa hivi punde unaashiria kuongezeka kwa mzozo kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu za nyuklia tangu shambulio la Jumanne.
“Tishio lolote kwa uhuru wa Pakistani na usalama wa raia wake litakabiliwa na hatua madhubuti za ulipizaji,” Kamati ya Usalama ya Kitaifa imeonya. Imefafanua zaidi: “Washauri wa ulinzi wa India, wanamaji na jeshi la anga huko Islamabad wanatangazwa kuwa watu wasiostahili”; “Biashara yote na India, ikijumuisha kwenda na kutoka nchi za tatu zinazopitia zinazopitia Pakistani, imesimamishwa mara moja.” Kwa kuongeza, “nafasi ya anga ya Pakistani itafungwa mara moja kwa mashirika yote ya ndege yanayomilikiwa na India.”
Kama India ilivyofanya siku moja kabla kwa raia wake, “Pakistani inasimamisha visa zote zinazotolewa kwa raia wa India na kuzifuta mara moja, isipokuwa zile za mahujaji wa kidini wa Sikh.” “Raia wa India kwa sasa nchini Pakistani wana saa 48 kuondoka nchini,” taarifa ya serikali imesema, na kuongeza kuwa kivuko kikuu cha mpaka sasa kimefungwa pande zote mbili.
Pakistani pia itatuma wito kwa ubalozi wa India, ametangaza Naibu Waziri Mkuu wa Pakistani Ishaq Dar, ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo.