
Unguja. Tatizo la maji safi na salama linalowakabili wananchi kisiwani hapa huenda likapata mwarobaini baada ya mradi mkubwa unaofadhiliwa na Benki ya Exim ya India kukamilika.
Kupitia mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani 92.18 (Sh237 bilioni) vimechimbwa visima 64 vinavyozalisha maji lita za ujazo milioni 177 kwa siku na yamejengwa matenki makubwa 15 yenye ujazo wa lita milioni 134 na kuweka mtandao wa usambazji wa maji kilometa 164.9.
Hata hivyo, licha ya mradi huo kukamilika kwa kujenga matenki, hatua inayoendelea sasa kwa baadhi ya maeneo ni kuwaungia wananchi maji hayo licha ya baadhi ya maeneo tayari hatua hiyo kukamilika.
Hayo yamebainika leo Alhamisi Februari 20, 2025 katika ziara maalumu ya ujumbe wa Serikali ya India kuangalia miundombinu hiyo na kueleza kuridhishwa huku wakiahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kushughulikia matatizo ya wananchi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Suja Menon amesema:“Tunafurahia kuona mradi umekamilika kwa viwango vinavyotakiwa, inaonesha jinsi gani India inavyobadilishana utaalamu na Zanzibar.”
“Tunaangalia zaidi mbele katika mafanikio yanayopatikana kwa ushirikiano huu kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Zanzibar,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa), Dk Salha Mohamed Kassim amesema mradi huo una thamani ya dola 92.18 milioni ulianza utekelezaji wake tangu mwaka 2021 ukiwa na skimu saba utanufaisha shehia 55, kati ya hizo 48 zipo Mkoa wa Mjini Magharibi na shehia mbili zipo Kaskazini na tano zipo Mkoa wa Kusini Unguja.
“Lengo ni kuhakikisha wananchi wote wanapata maji safi na salama,” amesema.
Amesema wapo katika mwaka wa mwisho kuangalia athari zinazoweza kujitokeza lakini mradi wameshakabidhiwa kwa hatua za awali na upo kwenye majaribio kwa mwaka mzima mpaka sasa.
Hata hivyo, Dk Salha amesema “Miradi ya maji kidogo ni migumu, kuyatafuta mpaka uyafikishe kwa wananchi lakini pamoja na changamoto zote ila tumefanikiwa.”
“Hatua iliyopo sasa ni kuwaunganishia watu maji kwenye majumba yao litakapomalizika hilo shehia 55 zitaanza kupata zote maji safi na salama na kuondokana na changamoto hiyo,” amesema.
Kuhusu kiwango kinachotolewa kwa sasa cha maji safi na salama kwa wananchi, Mkurugenzi huyo amesema: “Kwa sasa siwezi kusema kwa sababu kazi inaendelea kuunganisha watu mpaka ikikamilika ndio tutaweza kupata majibu kamili mpaka wakikamilika wote ndio tutaweza kutambua rasmi wananchi wanaopata maji ya Zawa watakuwa wangapi au usambazaji utakuwa umefikia asilimia ngapi.”
Hata hivyo, mpaka mwaka jana usambazaji wa maji katika kisiwa cha Zanzibar yalikuwa asilimia zaidi ya 70.
Nao baadhi ya wananchi katika shehia ya Maungani wamesema awali walikuwa wakipata maji kwa taabu lakini kwa sasa baada ya kuungiwa wanapata raha na neema
“Tunashukuru Mungu si haba maji tunapata, japo hayajafika katika maeneo yote bado wanafunga mita,” amesema Mwanaasha Khamis mkazi wa eneo hilo.
Sheha wa Shehia ya Maungani, Khamis Wazir Mwinshehe amesema wananchi wameupokea kwa furaha kubwa kwa sababu ya walikuwa na kilio cha kukosekana maji.
“Lakini sasa tunapata maji ya uhakika na tunaweza kujiamini kwamba maisha yetu yapo salama, maji haya yatasaidia pia kwenye kilimo,” amesema
Hata hivyo, ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali iendelee kuwafikishia wananachi wengine ambao bado miundombinu hiyo haijafika ili nao waweze kunufaika.