
Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza usitishaji vita kwa “ujumla na wa haraka” kati ya India na Pakistani siku ya , Mei 10. Maadui hao wawili wamehusika katika makabiliano makali ya kijeshi tangu siku ya Jumatano, na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora na kurushiana risasi kwenye mpaka wao unaozozaniwa huko Kashmir.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
India na Pakistan zimethibitisha kuidhinisha usitishaji huo wa mapigano, huku New Delhi ikisema “kulikuwa na mazungumzo ya moja kwa moja” kati ya nchi hizo mbili.
“India na Pakistani zimefikia makubaliano leo juu ya kusitisha mapigano na kusitisha operesheni za kijeshi,” Waziri wa Mambo ya Nje wa India Subrahmanyam Jaishankar amesema katika mkutano na waandishi wa habari.
“Baada ya usiku mrefu wa majadiliano ya upatanishi wa Marekani, ninayofuraha kutangaza kwamba India na Pakistani zimekubaliana USITISHWAJI MAPIGANO KWA UJUMLA NA HARAKA,” rais wa Marekani ameandika kwenye mtandao wake wa Truth Social, akitoa “pongezi zake kwa nchi zote mbili” kwa “mtazamo wao wenye kujenga na akili kubwa.”
Baada ya hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistani Ishaq Dar ametangaza kwamba Pakistanina India zimekubaliana “kusitisha mapigano na athari ya haraka” katika ujumbe kwenye X, kuthibitisha tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump. Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Pakistani pia imetangaza kuwa inafungua tena anga yake.
Lakini huko New Delhi, chanzo cha serikali ya India kimebainisha kwamba usitishaji mapigano umejadiliwa moja kwa moja kati ya India na Pakistani na kwamba majirani hao wawili hawakupanga kujadili chochote isipokuwa usitishaji wa mapigano.
Majadiliano mapya yapangwa kufanyika Mei 12
Usitishaji huo wa mapigano umejadiliwa kati ya mkuu wa operesheni za kijeshi wa Pakistani na mwenzake wa India wakati wa mazungumzo ya simu siku ya mchana, katibu wa wizara hiyo, Vikram Misri, amewaambia waandishi wa habari. “Viongozi wa operesheni za kijeshi watakutana tena Mei 12,” ameongeza.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema makubaliano hayo yalifuatia mazungumzo ya kina kati yake na Makamu wa Rais J.D. Vance, Mawaziri Wakuu wa India na Pakistani Narendra Modi na Shehbaz Sharif, na maafisa wengine wakuu.
“Ninafuraha kutangaza kwamba serikali za India na Pakistani zimekubali kusitisha mapigano mara moja na kuanza mazungumzo juu ya masuala mbalimbali katika eneo lisiloegemea upande wowote,” Rubio amesema kwenye ukurasa wake wa X. “Tunawapongeza Mawaziri Wakuu Modi na Sharif kwa hekima, busara, na ustadi wao katika kuchagua njia ya amani,” ameongeza.