Imani ya dini ya vijana Wakristo Ujerumani inapungua kulinganisha na ya vijana wa Kiislamu

Matokeo ya utafiti mpya uliofanywa na taasisi ya Ujerumani ya Shell Jugendstudie (Shell Youth Study) yanaonyesha kuwa, nafasi ya imani ya dini katika maisha ya vijana wa Kikristo nchini humo imepungua kwa kiasi kikubwa; na kinyume chake, utafiti huo unaonyesha kuwa, imani juu ya dini miongoni mwa vijana Waislamu ingali ni madhubuti na yenye umuhimu katika maisha yao ya kila siku.

Kwa mujibu wa utafiti huo, katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, imani juu ya Mungu miongoni mwa vijana Waislamu imeongezeka kutoka 72% hadi 79%.

Kushikamana na ufanyaji ibada za kila siku kwa vijana hao wa Kiislamu kumefikia kiwango cha 37% kwa kusali mara moja au zaidi kwa siku na 26% kwa wanaosali angalau mara moja kwa wiki. Ni 13% tu walioripoti kwamba hawasali kabisa.

Lakini kwa upande wa vijana Wakristo Wakatoliki ni asilimia 38 tu walioeleza katika utafiti huo kwamba imani juu ya Mungu ina umuhimu kwao, ikilinganishwa na asilimia 51 ilivyokuwa mwaka 2002.

Miongoni mwa vijana Waprotestanti, idadi hiyo imepungua kutoka asilimia 38 hadi 35.

Msikiti wa Cologne

Utafiti huo wa Shell Youth Study umeangazia pia kupungua kwa ushiriki wa vijana hao katika Kanisa na kueleza kwamba katika mwaka huu 2024, ni nusu tu ya vijana wenye umri wa miaka 12 hadi 25 wamejishughulisha na masuala ya Kanisa, idadi ambayo mwaka 2002 ilikuwa karibu theluthi mbili.

Ufa huu wa kushikamana na dini unaweza kuwa na athari kubwa kwa maingiliano ya kijamii na mtazamo juu ya mustakabali wa jamii ya Wajerumani.

Kwa kuongezeka idadi ya Waislamu nchini Ujerumani, leo hii idadi ya Misikiti na vituo vinavyoendesha shughuli zao kwa jina la Uislamu nchini humo imefikia 2,700, ambapo 300 kati yao ni vya Waislamu wa Kishia.

Japokuwa idadi ya Waislamu nchini Ujerumani imeongezeka kwa kiasi kikubwa na Waislamu wanazingatia zaidi masuala ya kidini kuliko Wakristo, kuenea kwa Uislamu nchini humo hakujaipendeza serikali ya Berlin na vyama vya mrengo wa kulia vyenye misimamo ya kufurutu mpaka.

Serikali ya Ujerumani inaviwekea vizuizi na hata kuvipiga marufuku vituo vikubwa vya Kiislamu kwa kisingizio cha kuwa na uhusiano na nchi za kigeni…/