Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia jinsi harakati za Muqawama wa Kiislamu za Hizbullah na HAMAS zinavyoendelea na mapambano yao kwa nguvu zote licha ya misukosuko mikubwa iliyozikumba harakati hizo na kusisitiza kuwa, kama inavyoonesha ahadi ya Allah, ushindi wa kambi ya Muqawama ni kitu cha lazima kisichoepukika.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo leo asubuhi wakati alipoonana na wajumbe wa Baraza la Wanachuoni Wataalamu (linalomchagua Kiongozi Muadhamu na kusimamia kazi zake) na kusisitza kuwa, matukio ya hivi karibuni yamezidi kuthibitisha kuwa ushindi wa kambi ya Haki na ya Muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni ni kitu cha lazima.
Vile vile amegusia jinsi mikono ya Marekani na nchi za Ulaya ilivyojaa damu za watu wasio na hatia kutokana na jinai zinazofanyika Ghaza na Lebanon na kusema kuwa, matokeo ya kuendelea jihadi imara huko Lebanon, Ghaza na Palestina ni ushindi wa kambi ya Haki na ya Muqawama. Kuna siku dunia na eneo hili litashuhudia jinsi utawala wa Kizayuni unavyoshindwa waziwazi na wanamapambano hao wa Kiislamu.

Aidha Imam Khamenei amesema, uzoefu wa miongo kadhaa iliyopita ya ushindi mbalimbali wa Muqawama mbele ya uvamizi wa Wazayuni ni ushahidi mwingine wa wazi wa kwamba mara hii pia, kambi ya haki ndiyo itakayoshinda. Amesema, katika kipindi cha karibu miaka 40 iliyopita, Hizbullah imekuwa ikipambana na utawala wa Kizayuni katika awamu na miji tofauti kama Beirut, Saida, Sur n.k, na hatimaye tumeona jinsi ilivyomlazimisha adui Mzayuni akimbie kutoka kwenye miji, vijiji na milima ya kusini mwa Lebanon.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema kuwa, kutokana na baraka, idili, subira na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu alikokuwa nako shahid Sayyid Hassan Nasrullah, mwanamapambano huyo amefanikiwa kuigeuza Hizbullah kutoka kundi dogo kuwa taasisi kubwa yenye nguvu za kupigiwa mfano ambayo imeweza kumlazimisha adui aliyejiandaa kwa silaha zote za kisasa kukimbia kwenye maeneo aliyokuwa akiyakalia kwa mabavu.
Aidha amesema, lengo la Wazayuni katika vita vyao vya hivi sasa ni kuiangamiza kikamilifu HAMAS, lakini pamoja na kwamba Wazayuni wamefanya mauaji ya umati ya makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia na pamoja na kuwaua shahidi viongozi wa HAMAS na Hizbullah, lakini hakuna tija yoyote aliyopata adui isipokuwa kuzidi kuaibika, kuzidi kuchukiza, kuzidi kulaaniwa na kuzidi kutengwa duniani. Adui ameshindwa kufikia malengo yake, na HAMAS bado iko imara kwenye medani za mapambano na huu ni ushahidi mwingine wa kushindwa utawala wa Kizayuni.