Imam Khamenei: Netanyahu ahukumiwe kifo, hukumu ya ICC ya kukamatwa mhalifu huyo wa vita haitoshi

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ametoa wito wa kuhukumiwa kifo Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye hati ya kukamatwa kwake imetolewa na Mahakama ya kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutokana na mauaji ya kimbari ya utawala huo ghasibu huko Gaza na nchini Lebanon.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo katika hadhara ya matabaka mbalimbali ya jeshi la kujitolea la Basiji la Iran na kueleza kuwa fikra za Basiji zinatokana na misingi miwili yaani “kumwamini Mwenyezi Mungu” na “kujiamini”. 

“Waranti ya (ICC) wa kukamatwa Netanyahu hautoshi, hukumu ya kifo ya Netanyahu lazima itolewe,” amesema Ayatullah Khamenei.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu yenye makao yake makuu The Hague (ICC) imetoa hati za kukamatwa Netanyahu na waziri wake wa zamani wa vita, Yoav Gallant kutokana na uhalifu wao wa kivita unaohusiana na mauaji ya kimbari yanayoendelea Gaza.

Akizungumzia uvamizi wa Israel katika Ukanda wa Gaza na Lebanon, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kushambulia nyumba za raia kwa mabomu sio ushindi bali ni “uhalifu”.

“Adui hajashinda vita dhidi ya Gaza na Lebanon, na kamwe hataweza kufanya hivyo”, amesisitiza Ayatullah Khamenei.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja hatua ya Basiji ya kung’amua njama za Marekani katika nchi za eneo la Magharibi mwa Asia na kusimama kidete dhidi ya njama hiyo kuwa ni sababu nyingine ya kuimarisha Basiji katika uga wa kisiasa na kusema: Ili kulinda maslahi yake katika eneo hilo, Marekani inaanzisha tawala za “kidhalimu na kidikteta” au “machafuko na ukiukaji wa sheria.”

Amesema, kinyume na matakwa ya wahalifu, jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza na Lebanon zimepelekea kuimarika na kushadidisha mapambano na Muqawama na kuongeza kuwa: Kijana mwenye ari wa Palestina na Lebanon kutoka matabaka yote, anapoona kwamba anakabiliwa na hatari ya kifo, sawa awe kwenye medani ya vita au la,  huelewa kwamba hana chaguo jingine isipokuwa kupambana; Kwa hivyo wajinga wahalifu wanastawisha zaidi Kambi ya Muqawama na mapambano  kwa mikono yao wenyewe.