Katika mazingira yenye ushindani mkubwa wa sekta ya fedha nchini Tanzania, ambapo changamoto za kiuchumi ni nyingi kuliko inavyodhaniwa, benki moja imeibuka kama mfano wa uvumilivu, ubunifu, na ukuaji wa mageuzi. Nayo si nyingine bali I&M Bank Tanzania.
Kwa mafanikio makubwa iliyoyapata mwaka 2024 na mwanzo wa kasi wa mwaka 2025, I&M Bank siyo tu kwamba haiko mbali kuzifikia benki kubwa kwa kasi ya ukuaji wake, bali inabadilisha dhana nzima juu ya kile benki za madaraja ya kati nchini zinaweza kufanya kwa ubora.

I&M Bank Tanzania yasherehekea miaka 50 ya taasisi hiyo.Sherehe hizo ziliambatana na ufunguzi wa ofisi za makao makuu yake mapya yaliyopo Masaki, Dar es Salaam.
Ikipewa nguvu na dira thabiti, ubunifu wa kidijitali wa hali ya juu, na msisitizo usiyoyumba katika kulinda thamani ya wateja, I&M Bank Tanzania inaendelea kujitengenezea mazingira mazuri ya kuwa miongoni mwa taasisi za fedha zenye ushawishi mkubwa nchini.
Mafanikio ya 2024: Hadithi ya ukuaji
Takwimu zinaeleza yote. Mwaka 2024, I&M Bank Tanzania ilichapisha taarifa za kifedha za kuvutia zaidi zilizoonyesha ukuaji maradufu ambapo faida kabla ya kodi ilifika Sh bilioni 18.3, ikiwa ni ongezeko la asilimia 242 ikilinganishwa na mwaka uliopita, huku mali zote za benki zikifikia Sh bilioni 804, sawa na ongezeko la asilimia tisa.
Pia, mtaji wa wanahisa ulikua kufikia Sh bilioni 119, ukionyesha ongezeko la asilimia 14. Mapato ya riba yalipanda hadi Sh bilioni 97, sawa na ongezeko la asilimia 35. Mikopo chechefu ilishuka hadi asilimia 8.4, ushukaji wa asilimia 51, ikiashiria usimamizi madhubuti wa kitabu cha mikopo.
“Matokeo ya 2024 ni ujumbe thabiti wa dhamira yetu,” alisema Zahid Mustafa, Mkurugenzi Mtendaji wa I&M Bank Tanzania. “Hatuwezi kusema tu kuwa tunakua—bali tunajenga urithi wa uaminifu, ubunifu na ustawi wa pamoja.”
Robo ya Kwanza ya 2025: Ukuaji wa kasi zaidi
Mafanikio haya hayakuishia mwaka 2024 pekee, yalibisha hodi hadi mwaka 2025. Katika robo ya kwanza pekee, faida kabla ya kodi ilifikia takribani Sh bilioni 6.3, ikiwa ni ongezeko la asilimia 151 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024.

Mfanyakazi wa I&M Bank Tanzania akimhudumia mteja maeneo ya Posta, Kinondoni, Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja.
Amana za wateja ziliongezeka kufikia Sh bilioni 668, sawa na ongezeko la asilimia 14. Mikopo halisi na malipo ya awali yalipanda kufikia Sh bilioni 521, sawa na ukuaji wa asilimia 12, huku mtaji wa wanahisa ukipanda hadi Sh bilioni 124, sawa na ongezeko la asilimia 17.
Licha ya changamoto za kiuchumi zilizopo, I&M Bank imeendelea kudhibiti hatari kupitia mikakati madhubuti ya uboreshaji mikopo, na usimamizi wa hatari na mifumo ya urejeshaji, hatua zilizosaidia kuimarisha jalada lake la mikopo.
Ubunifu wa Kidijitali: Kuchochea ukuaji jumuishi
Katika msingi wa mafanikio ya I&M Bank mageuzi ya kidijitali yana nafasi kubwa. Kupitia bidhaa yake mashuhuri hivi sasa iitwayo ‘Kamilisha,’ iliyoanzishwa kwa ushirikiano na Airtel Tanzania.
I&M Bank imekuwa ikijielekeza zaidi kwenye kuhudumia wateja wakubwa huku mkazo zaidi ukiwa kwenye nyanja za wateja wadogo na wajasiriamali ambao ndiyo injini ya ukuaji wa benki. Miongoni mwa masuluhisho ya benki ni pamoja na:
- Uzinduzi wa Huduma ya Kuhamisha Fedha Kutoka Benki kwenda Kwenye Simu: Benki hivi karibuni imeondoa rasmi makato kwenye huduma ya kuhamisha fedha kutoka benki kwenda kwenye simu kwa wateja wadogo na wajasiriamali wadogo na kati kupitia kampeni ya Ni Bure Kabisaaa ambayo inaifanya I&M kuwa benki pekee inayotoa huduma hiyo nchini. Huduma hii itawawezesha wafanyakazi wenye mishahara na kampuni kuokoa fedha kupitia mitandao yote ya simu.
- Programu tumishi (App) mpya ya simu za mkononi na huduma ya Benki Mtandao: Huduma ambayo husaidia kupata huduma zote za kibenki kwa urahisi sambamba na uwepo wa vipengele vingi vya machaguo kwa wateja wake wadogo na wakubwa.
- Rafiki Chat Banking: Huduma ya kipekee inayowawezesha wateja kufanya miamala kupitia WhatsApp, kwa kutumia teknolojia ya Akili Mnemba.
- Uzinduzi wa Akaunti ya Biashara ya ZAIDI: Hii ni akaunti mpya ya biashara maalumu kwa ajili ya wajasiriamali wadogo na kati ambayo inawapa riba wateja hao kwenye masalio ya akaunti zao wanapoweka fedha.
“Sisi si benki pekee, ni mfumo wa kidijitali unaowafuata wateja walipo,” alisema Mkuu wa Idara ya Wateja Wadogo na Huduma za Benki Kidijitali, Simon Gachahi. “Ubunifu wetu unalenga kuondoa vikwazo, kuleta ujumuishi wa kifedha, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania.”
Kuwainua wajasiriamali wadogo, kati na kampuni kubwa kwa pamoja
Dhamira ya I&M Bank katika kuimarisha uchumi wa Tanzania kupitia wajasiriamali wadogo na wa kati haibadiliki. Mwaka 2025, benki ilizindua bidhaa mbili mpya za biashara ambazo ni Akaunti ya Biashara ya ZAIDI na Akaunti ya Biashara ya Moja, baada ya utafiti wa kina wa mahitaji ya wateja.
“Wajasiriamali wadogo na wa kati ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, kukiwa na zaidi ya biashara milioni tatu zinazochangia asilimia 27-35 ya Pato la Taifa na kuajiri watu zaidi ya milioni tano. I&M Bank Tanzania, tunaamini katika kuwawezesha kwa suluhisho za kifedha bunifu zinazochochea ustawi wa pamoja,” anaeleza Meneja.
Dira: Kuwa Benki Daraja la 1 Ifikapo 2026
Ndoto za I&M Bank Tanzania haziishii hapa. Kwa lengo la kufikia hadhi ya daraja la kwanza (Tier 1) ifikapo mwaka 2026, benki inawekeza kwa kiwango kikubwa katika teknolojia, rasilimali watu, na ubunifu unaomlenga mteja.
“Shauku na bidii ya timu yetu ndiyo nguvu ya mafanikio yetu,” alisema Mustafa. “Pamoja na wateja na wadau wetu, tunajenga benki isiyoishia kushindana, bali inaongoza.”
Zaidi ya Benki: Kichocheo cha maendeleo
Safari ya I&M Bank Tanzania ni simulizi ya ndoto kubwa, uimara na matokeo chanya. Kwa kuendeleza ujumuishi wa kifedha, kuwawezesha wajasiriamali na kuwekeza katika teknolojia, benki hii haijafanikiwa tu, bali inatengeneza kesho mpya ya sekta ya kifedha nchini.
Kadri inavyoendelea kuvuka matarajio na kuweka viwango vipya, jambo moja liko dhahiri kwa kila mmoja wetu: I&M Bank Tanzania siyo benki inayokua kwa kasi tena, bali ni taasisi kubwa ya kifedha ambayo imejipanga vilivyo kuiongoza sekta ya fedha katika muongo mpya wa ustawi zaidi.
Kwa maelezo zaidi kuhusu bidhaa na huduma za I&M Bank Tanzania, tembelea: www.imbank.com/tz