
Unguja. Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kwa mwaka wa fedha 2025/26 imepanga kutekeleza malengo makuu manane, ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula.
Akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo barazani leo Mei 17, 2025 Waziri mwenye dhamana, Shamata Khamis Shaame ameomba baraza kuidhinisha Sh92.728 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa malengo hayo.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2025/26 wizara imepanga kutekeleza miradi 13 ambayo inaombewa Sh58.183 bilioni kati ya fedha hizo Sh24.7 bilioni kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Sh33.482 bilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Amesema wataimarisha utoaji wa huduma za kilimo, maliasili na mifugo ikiwamo ujenzi wa vituo viwili vya kutolea huduma, kimoja Unguja na kingine Pemba.
“Tunalenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ikiwamo ndizi na mpunga, mboga na matunda, asali na uzalishaji wa mazao ya mifugo kwa kufanya tafiti, utaalamu na usambazaji teknolojia kwa wakulima,” amesema.
Amesema takwimu zinaonyesha eneo lililopandwa mazao ya kilimo kwa mwaka 2024 limepungua hadi kufikia ekari 104,667.8 ikilinganishwa na ekari 122,514.2 za mwaka 2023, sawa na upungufu wa ekari 17,846.4.
Waziri amesema uzalishaji wa mazao ya kilimo umepungua kwa tofauti ya tani 144,870.8 kutoka tani 527,800 mwaka 2023 ikilinganishwa na tani 382,929.2 mwaka 2024.
“Upungufu huo umetokana na kuwapo vipindi virefu vya mvua na jua visivyotabirika.” amesema.
Ameeleza wizara imekuwa ikifanya jitihada kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji tangu mwaka 2017 na kwamba hadi sasa eneo lililowekewa miundombinu ya umwagiliaji limefikia ekari 5,750 (sawa na hekta 2,300).
Uzalishaji wa mpunga umeshuka kwa tani 2,256.8 kutoka tani 43,658.8 mwaka 2023 hadi tani 41,402.0 mwaka 2024 hii ni kutokana na eneo kubwa la mpunga la Zanzibar hutegemea mvua.
Hata hivyo, amesema mwaka 2024 uzalishaji mpunga wa kutegemea mvua umepungua kutoka tani 36,362.4 hadi tani 29,767.5.
Kwa upande wa karafuu ambalo ni zao la biashara amesema uzalishaji umepungua kutoka tani 2,654.6 mwaka 2023 hadi kufikia tani 1,167.4 za mwaka 2024 ikiwa ni sawa na upungufu wa asilimia 56.
“Hali hii imetokana na kuwa na msimu mdogo wa uzalishaji na uwepo wa mvua kubwa,” amesema.
Amesema wizara itaendelea kutoa huduma za ukulima na zana za kilimo kwa wakulima na ushajihishaji wa sekta binafsi.
Akizungumzia upandaji miti amesema wameotesha miche 1.7 milioni ya misitu, mikarafuu, minazi, matunda na viungo.
Katika kuimarisha kilimo, amesema Serikali inatarajia kufanya ukarabati wa mabonde 10 ya umwagiliaji maji ya Mtwango, Mwera, Bumbwisudi, Kibokwa, Kianga, Saninga, Kinyakuzi, Weni, Makombeni na Tibirinzi.
Pia ukarabati wa visima na pampu katika mabonde ya umwagiliaji maji na kuendeleza kilimo cha umwagiliaji maji kwa njia ya matone.
Ili kuongeza upatikanaji wa mazao ya karafuu na nazi, wizara inatarajia kuzalisha miche 700,000, kati ya hiyo 200,000 ni minazi na 500,000 ya mikarafuu. Miti hiyo itagawiwa kwa wakulima.
Amesema watafanya ukarabati na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia akiba ya chakula, kufanya tathmini uzalishaji wa mpunga na kusimamia uzalishaji wa mbegu bora za nafaka sambamba na kudhibiti milipuko ya wadudu na maradhi ya mimea.
Katika sekta ya misitu, wizara inatarajia kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi wanaotembelea hifadhi kutoka 64,000 hadi kufikia 100,000 kwa kuimarisha vivutio na kuhamasisha miradi ya uwekezaji katika maeneo ya hifadhi za misitu kwa lengo la kuongeza mapato.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Biashara na Kilimo, Hussein Ibrahim Makungu amesem kamati inaunga mkono juhudi na mikakati iliyowekwa na wizara yenye lengo la kuendeleza kilimo biashara ili kuzidisha uzalishaji wa mazao ya chakula.
“Mafanikio ya mikakati hii itakua ndiyo chachu ya kuongeza uzalishaji na hatimaye itapunguza utegemezi wa chakula kutoka nje,” amesema.
Hata hivyo, amesema bado wanaendelea kupata malalamiko kutoka kwa wakulima kuhusu vitendo vya baadhi ya wafugaji kuingiza wanyama katika mabonde.
Kamati imeshauri wizara itenge fungu kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na kukaa na jumuiya za wafugaji kuwapatia elimu juu ya madhara yanayoweza kujitokeza pindi mifugo ikizagaa ndani ya maeneo ya miradi.