Ikangalombo na nafasi tatu Yanga

Yanga haikuwa na mawazo sana na michuano ya kimataifa wakati ikimsajili kiungo  Jonathan Ikangalombo kutoka AS Vita.

Timu hiyo ya Jangwani ilitangaza kumtaka mchezaji huyo kuanzia mwanzoni mwa msimu lakini ikashindwa kumpata na bahati mzuri ikafanikiwa kukamilisha usajili wake kwenye dirisha dogo, siku chache kabla haijacheza mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Al Alger na kuambulia suluhu ambayo iliwafanya waondolewe kwenye michuano hiyo.

Usajili wa winga huyo anayemudu kucheza pia eneo la ushambuliaji ni jibu kuwa Yanga inataka kuhakikisha kuwa inachukua ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo na kuendelea kuweka rekodi zake sawa, faida kubwa ambayo Yanga wanakutana nayo ni kwa kuwa mchezaji huyo ana uwezo wa kutumika kwenye maeneo matatu tofauti.

Ni winga wa kushoto, sehemu ambayo Yanga imekuwa na wachezaji tofauti tofauti, winga wa kulia na eneo la ushambuliaji ambalo Yanga pia imekuwa ikihaha kupata mchezaji sahihi wa kutimka kwenye eneo hilo kutokana na Prince Dube na Kennedy Musonda kushindwa kufanya vizuri kwenye nafasi hiyo kwa msimu huu.

Yanga imemsajili mchezaji huyo  kwa mkataba wa miaka miwili akiwa anatajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji wenye kasi lakini pia akiwa na umbo kubwa ambalo linaweza kuwa faida nyingine kwa timu hiyo ya Jangwani.

Usajili wa staa huyo raia wa DR Congo umeilazimisha Yanga kuachana na aliyekuwa mshambuliaji wake, Jean Baleke ili kukidhi mahitaji ya wachezaji 12 wa kimataifa kwenye timu hiyo.

Ikangalombo kwenye michezo aliyoitumikia Vita kabla ya kujiunga na Yanga alionekana kuwa mchezaji mwenye kasi, uwezo mzuri wa kupiga pasi na mashuti makali, jambo ambalo linaonekana kuwa anaweza kuwa na namba nzuri kwenye michezo ya Ligi Kuu pamoja na Kombe la FA iliyobaki.

Ikangalombo mwenye miaka 22 ni umri sahihi wa wachezaji wa kisasi ambao wanaweza kutumika kwenye klabu kwa muda mrefu,jambo lingine ambalo linaonekana kuwa na faida kubwa kwenye kikosi hicho cha kocha Saed Ramovic ambaye amekuwa akipambana kujenga timu bora ambayo inaweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Kipindi hiki ambacho Yanga inaonekana kuwakosa baadhi ya wachezaji wake mahiri kutokana na majeraha akiwemo Maxi Nzengeli, inaonekana kuwa ni nafasi ya moja kwa moja kwa mchezaji huyo kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kama kocha wa timu hiyo ataridhishwa na kiwango chake mazoezini.

Wasifu wake unaonyesha kuwa siyo mchezaji mwenye jina kubwa sana akiwa ameanzia soka lake kwenye kikosi cha DC Motema Pembe na mwanzoni mwa mwaka jana akajiunga na Vita ambayo hakutumika kwenye michezo mingi ukiacha miwili ya Kombe la Shirikisho ambayo alicheza kwa dakika zote 180 na kuonyesha uwezo wa juu.

Kuonyesha kuwa ni mmoja kati ya wachezaji bora, pamoja na kutokuwa na jina kubwa, lakini ameshafanikiwa kuichezea timu ya Taifa ya DR Congo michezo miwili, likiwa ni moja ya taifa ambalo linatumia wachezaji wengi kutoka nje ya nchi yao.

Jambo la msingi ni kusubiri kuona makali yake wakati Ligi Kuu Bara itakaporejea mwanzoni mwa mwezi ujao baada ya michuano ya CHAN kusogezwa mbele.