Ikanga Speed aiomba Dabi ya Kariakoo

YANGA imerudi kazini kuanza maandalizi ya kwenda kupambana na watani wao Simba waliorejea jijini Dar es Salaam juzi ikitokea Arusha, ilipoenda kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union, lakini kocha wa vinara hao, Miloud Hamdi akashtua kuwa zile dakika 21 alizompa winga mpya, Jonathan Ikangalombo ‘Ikanga Speed’, jamaa kama kanogewa.

Lakini kama unawaza kanogewa nini, chama hilo la Jangwani limeendelea na mazoezi makali kujiandaa na mchezo huo wa dabi, lakini mastaa kila mmoja akijaribu kuingia kichwani mwa kocha huyo ili amsaidie kwenye mchezo huo kupata ushindi.

Jambo la kushangaza zaidi ni kwamba, Kinga Speed ana spidi kwelikweli na sasa anawataka Simba.

Yanga inatarajiwa kuwa wenyeji wa Dabi ya Kariakoo itakayopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku kocha Hamdi akiwatuliza wanayanga kwa ajili ya mchezo huo wa 114 wa Ligi y Bara tangu 1965.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Hamdi amesema alifurahishwa na dakika 21 za kwanza za Ikanga Speed alizocheza dhidi ya Pamba Jiji katika mechi iliyopita iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, wakati Yanga ikishinda kibabe kwa mabao 3-0, lakini kumbe winga huyo ilipomalizika mechi hiyo, akaomba apewe muda zaidi katika mechi dhidi ya Simba.

Hamdi amesema winga huyo alionyesha mwanzo mzuri, akithibitisha kwamba ni mchezaji anayestahili kuvaa jezi za timu hiyo, akionyesha ukomavu mkubwa wa kuhimili presha na ujasiri wa kufanya mambo makubwa ndani ya mechi ya kwanza.

Winga huyo, aliingia katika mchezo huo wa Ligi Kuu dhidi ya Pamba dakika ya 69, akionyesha kasi nzuri, ubora wa kutoa pasi na kuhusika kwenye matukio makubwa ya mchezo akishiriki kutengeneza bao la pili la mchezo huo.

“Jonathan, (Ikangalombo) nilikuwa nasema wakati wote ni mchezaji mzuri mwenye ubora mkubwa, muda ambao tulimpa juzi (Ijumaa iliyopita), ulikuwa mchache lakini nadhani watu waliokuwa na maswali wameona kuna kitu gani anacho,” amesema Hamdi na kuongeza:

“Mechi ilivyokwisha nilimuita na kumwambia amefanya vizuri, lakini akaniambia anataka sana kucheza mechi ijayo dhidi ya Simba, nimemwambia asubiri tutaona nini tutaamua kwa kuwa hiyo ni mechi yenye hesabu nyingi, ila naamini hata akicheza atafanya kitu kikubwa kwa kuwa ni mchezaji mkubwa.”

SHUNGU ATIA NENO
Kocha msaidizi wa AS Vita, Raoul Shungu anayotoka Ikanga Speed amemuondoa wasiwasi Hamdi akisema hatashangaa kuona winga huyo anafanya kitu kikubwa kama atacheza dhidi ya Simba.

Shungu ambaye amewahi kufanya kazi Yanga, alisema Ikanga Speed ni mchezaji mkubwa aliyecheza mechi kubwa za watani wa jadi na kwamba anavyowajua mashabiki wa Yanga wanavyojaa uwanjani kama winga huyo atapata nafasi atafanya kitu tofauti.

“Nimeona amecheza mechi iliyopita, nilisikia alitakiwa kupunguza uzito, inawezekana kwa kuwa hapa alisimama kucheza kwa muda wakati analazimisha kuondoka, lakini nimemuona amerudi kwenye mwili wake,” amesema Shungu.

“Kama kocha wa Yanga hapo atampa muda wa kucheza dhidi ya Simba atafanya vizuri sana, nadhani mashabiki wa Yanga wataona ubora wake na kama wakijaa vizuri uwanjani hilo ndio wachezaji Wakongomani wanataka atajituma sana kufanya mambo makubwa.”

Ikanga Speed alitua Yanga kupitia dirisha dogo na alikuwa hajatumika kwa mchezo wowote tangu enzi za kocha Sead Ramovic na hata alipokuja Hamdi ambaye alimpa dakika 21 dhidi ya Pamba Jiji na kukata kiu ya mashabiki wa timu hiyo waliokuwa na hamu ya kumuona uwanjani.