Ijumaa, tarehe 8 Novemba, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 6 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1446 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 8 Novemba 2024.

Siku kama ya leo miaka 368 iliyopita, alizawa Edmond Halley, mtaalamu wa nyota wa nchini Uingereza.

Halley alisoma katika kitengo cha Queen kilicho chini ya chuo kikuu cha Oxford, nchini humo na kuanza kujishughulisha na masuala ya utafiti wa nyota akiwa kijana mdogo, huku akifanya safari kuelekea kusini mwa dunia kwenye kisiwa kilichoko Bahari ya Atlantic.

Edmond Halley alichukua muda mwingi katika kutalii nyota ambapo aligundua kwamba, kama ilivyo kwa sayari, nyota nazo zina obiti za duara dufu na kwa msingi huo wakati wa kurudi kwao unaweza kuhesabika. Mwaka 1704 alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Oxford. Mnamo 1720, aliteuliwa kuwa mnajimu katika Royal Observatory huko Greenwich. Halley alifariki dunia mwaka 1742.   

Edmond Halley

Katika siku kama ya leo miaka 350 iliyopita, alifariki dunia John Milton, malenga wa Kiingereza.

Kazi za kwanza za ushairi za John Milton zilijulikana kwa majina ya Roho ya Huzuni na Roho ya Furaha. Kazi nyingine ya uandishi ya John Milton ni ile aliyoipa jina la Paradise Lost.

Malenga Milton alikuwa akitetea suala la kutenganishwa serikali na kanisa, kuweko uhuru wa kuabudu na wakati huo huo aliunga mkono uchujaji wa taarifa uliokuwa ukifanywa na serikali. 

John Milton

Siku kama ya leo miaka 129 iliyopita sawa na tarehe 8 Novemba mwaka 1895, miale ya X iligunduliwa na Wilhem Conrad Rontgen, mwanafizikia na mwanasayansi maarufu wa Ujerumani.

Mtaalamu huyo mwaka 1901 alitunukiwa tuzo ya Nobel kwa kufanikiwa kugundua miale hiyo. Kwa kuwa hakutambua miale aliyoigundua, Rontgen aliamua kuipa jina la X.

Miale hiyo hupenya kwa urahisi katika mwili wa mwanadamu na kwa ajili hiyo ni njia nzuri zaidi ya kuchukua taswira ya viungo au picha ya X-ray inayotumiwa kujua sehemu za ndani ya mwili zilizodhurika au kuvunjika. 

Wilhem Conrad Rontgen

Siku kama ya leo miaka 124 iliyopita alizaliwa Bi Margaret Mitchell mwandishi wa Kimarekani huko Atlanta katika jimbo la Georgia nchini humo.

Baba yake Bi Mitchell alikuwa wakili wa mahakama. Kwa muda fulani alisomea fani ya udaktari, lakini baadaye alilazimika kukatisha masomo hayo kutokana na majonzi aliyokuwa nayo kufuatia kifo cha baba yake. Margaret allianza kazi ya uandishi akiwa na miaka 22.

Alizidi kupata umashuhuri baada ya kuchapisha riwaya yake aliyoiita kwa jina la “Gone with The Wind.”

Margaret Mitchell

Katika siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, Sheikh Nusratullah Ansari mwanamapambano wa kimapinduzi wa Iran alikufa shahidi kutokana na mateso ya makachero wa Shirika la Usalama wa Taifa la utawala wa Shah lililojulikana kwa jina la SAVAK.

Hujjatul Islam Nusratullah Ansari alizaliwa huko Buin Zahra. Sambamba na masomo yake ya Hawza alikuwa akiendesha pia harakati za mapambano ya kisiasa dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Shah nchini Iran.

Hatimaye alitiwa mbaroni mwaka 1354 Hijria Shamsia na kufa shahidi katika siku kama ya leo baada ya miezi sita ya mateso.   

Sheikh Nusratullah Ansari