Ijumaa, tarehe 18 Oktoba, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 14 Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria sawa na 18 Oktoba 2024.

Siku kama ya leo miaka 1380 iliyopita Mukhtar bin Abi Ubaida al-Thaqafi alianza mapambano ya kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein bin Ali (a.s), mjukuu wa Mtume Muhammad SAW.

Mwaka 61 Hijria Imam Hussein (as) akiwa pamoja na wafuasi na watu wa familia yake, aliuawa shahidi na jeshi la Yazid akiwa katika harakati za kuilinda dini tukufu ya Uislamu. Mukhtar alianzisha harakati zake za mapambano katika mji wa Kufa. Kabla yake, kulijitokeza kundi la ‘Tawwabiin’ ambalo lilipigana na utawala wa Bani Umayyah, kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein AS.

Mukhtar Thaqafi alitawala Kufa kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja na mwishowe alishindwa na jeshi la Mus’ab bin Zubair na kuuawa shahidi.

Kaburi la Mukhtar bin Abi Ubaida al Thaqafi

Miaka 157 iliyopita katika siku kama ya leo, ardhi ya Alaska ilidhibitiwa na Marekani.

Alaska ni ardhi yenye upana wa karibu kilometa mraba milioni moja na laki tano, huko kaskazini magharibi mwa Amerika, ambapo hii leo ni moja ya majimbo ya nchi hiyo. Hadi mwaka 1867, Alaska ilikuwa ikidhibitiwa na Russia, hata hivyo katika kipindi hicho mfalme wa wakati huo wa Urusi ya zamani hakutilia maanani umuhimu wa ardhi hiyo na hivyo mwezi Oktoba mwaka 1867  akaamua kuiuza kwa Marekani.

Ni vyema ifahamike kuwa, hii leo Alaska inahesabika kuwa moja ya majimbo tajiri sana ya Marekani ambapo mwaka 1960 kulivumbuliwa mafuta na kuanza kuchimbwa katika eneo hilo hadi leo.   

Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita alifariki dunia msomi wa Uingereza na mvumbuzi wa mashine ya kikokoteo (Calculator) kwa jina la Charles Babbage.

Mwaka 1812 Miladia, Babbage aliasisi taasisi ya uchunguzi kwa ajili ya kuendeleza elimu ya hisabati na akiwa na umri wa miaka 24 akateuliwa kujiunga na taasisi ya ufalme ya Uingereza. Ni baada ya hapo ndipo akaanzisha harakati ndefu za utafiti wa kuunda mashine hiyo ya hesabu ambapo hadi kufikia mwaka 1833 Miladia akafanikiwa kuvumbua chombo hicho ambacho kilikuja kuwa mashuhuri kwa jina la Babbage.

Baada ya hapo karne moja baadaye wasomi mbalimbali waliifanyia marekebisho muhimu mashine hiyo sanjari na kuifanya itumie nishati ya umeme. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Charles Babbage akatambuliwa kwa jina la baba wa kikokoteo (Calculator).   

Charles Babbage

Miaka 102 iliyopita katika siku kama ya leo, Redio ya BBC iliasisiwa huko Uingereza.

Redio ya BBC awali ilikuwa ya mtu binafasi, lakini mwaka 1927 redio hiyo iliwekwa chini ya usimamizi wa serikali na ikamilikiwa na serikali ya London. Bajeti ya redio za BBC ambazo zinatangaza kwa lugha mbalimbali za dunia inadhaminiwa na serikali ya Uingereza.

Licha ya kuwa BBC inadai kwamba haipendelei upande wowote katika matangazo yake, lakini katika kipindi cha nusu karne ya hivi karibuni, chombo hicho cha kupasha habari kimegeuka na kuwa wenzo wa propaganda wa serikali ya Uingereza na hivyo kuiandalia London uwanja wa kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. 

Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita, msomi aliyegundua umeme, Thomas Edison, alifariki dunia.

Edison alizaliwa mwaka 1847 huko Marekani. Thomas Edison hakuwa na taalumu yoyote kutoka chuo kikuu bali ni tafiti na majaribio yake mengi ndiyo yaliyopandisha juu kiwango chake cha elimu na maarifa.

Akiwa kijana, Edison aliasisi maabara ya masuala ya kemia na kufanya majaribio makubwa katika maabara hiyo. Bidii ya msomi huyo ilimuwezesha kuvumbua mambo mengi ambapo muhimu kati ya hayo ni hatua yake ya kuvumbua umeme, kutengeneza lampu na gramafoni au santuri.   

Thomas Edison

Katika siku kama ya leo miaka 37 iliyopita manowari za jeshi la Marekani zilishambulia visiwa vya mafuta vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Ghuba ya Uajemi wakati wa vita vya Iraq dhidi ya Iran.

Mashambulizi hayo yalifanyika baada ya Kuwait iliyokuwa ikiusaidia utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein katika vita vyake dhidi ya Iran, kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu kuwa imeshambulia meli yake ya mafuta. Marekani ilivishambulia visiwa vya mafuta vya Iran kwa madai kuwa meli ya Kuwait iliyoshambuliwa na Iran ilikuwa na bendera ya nchi hiyo.