
Leo naendelea na mfululizo wa makala zangu elimishi kuhusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT), nikilielekeza jicho langu kwa Bunge.
Kwa mujibu wa Ibara ya 62 ya Katiba, JMT itakuwa na Bunge ambalo litaundwa na sehemu mbili: Rais na Wabunge.
Hii ina maana kwamba, japo Bunge ni mhimili unaojitegemea, Rais wa Tanzania bado ni sehemu yake.
Ndiye anayeunda Bunge, kulivunja, kumteua Mtendaji Mkuu wa Bunge, na kuidhinisha sheria zinazotungwa ili ziwe sheria halali za nchi.
Kwa hali hiyo, ingawa Spika ndiye mkuu wa mhimili wa Bunge, Rais ana mamlaka makubwa zaidi ambayo hayajitokezi moja kwa moja.
Kauli ya Hayati Rais John Magufuli kuhusu ‘mhimili uliojichimbia chini zaidi” inaweza kuhusiana na hali hii, ingawa si jambo linaloonekana wazi kwa wengi.
Nasema hivyo kwa sababu Ibara ya 63 ya Katiba inatamka kuwa Bunge ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano chenye madaraka ya kuisimamia na kuishauri serikali kwa niaba ya wananchi.
Na Bunge lina kazi kuu mbili ambazo ni kutunga sheria na kuisimamia Serikali.
Na majukumu haya yanafafanuliwa zaidi kama kumhoji waziri yeyote kuhusu masuala ya umma yanayohusu wizara yake, kujadili utekelezaji wa kila wizara wakati wa mkutano wa bajeti wa kila mwaka na kujadili na kuidhinisha mipango ya maendeleo ya muda mrefu na mfupi na kutunga sheria za kusimamia utekelezaji wake.
Lakini pia kutunga sheria pale inapohitajika na kujadili na kuridhia mikataba inayohusu Jamhuri ya Muungano ambayo inahitaji ridhaa ya Bunge.
Bunge la sasa lilikuwa likiitwa Baraza la Kutunga Sheria enzi za ukoloni, likiwa na jukumu lake kuu la kutunga sheria.
Hivyo, mtunga Katiba aliposema kazi ya Bunge ni kutunga sheria, alikusudia kuwa Bunge kama chombo kikuu cha nchi, linapaswa kutunga sheria kwa niaba ya wananchi.
Hata hivyo, inapotokea serikali inahitaji sheria fulani, hulielekeza Bunge kuitunga.
Lakini mchakato wa kutunga sheria kama inavyoelekezwa na Kanuni za kudumu za Bunge, hususan Ibara ya 80, zinaainisha kuwa kuna aina mbili za miswada ya sheria ambayo ni wa Serikali na ile Binafsi.
Na tunaelezwa kwamba kila muswada lazima utangazwe katika Gazeti rasmi la Serikali angalau mara mbili na kuwepo kwa muda wa angalau wa siku saba kati ya matangazo hayo.
Na tangazo la kwanza lazima litangazwe angalau kwa siku 21 kabla ya muswada kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni.
Ila kwa muswada wa dharura wa Serikali, hauwezi kujadiliwa bila kibali rasmi cha Rais kinachothibitisha kuwa ni wa dharura.
Mbunge yeyote au Kamati ya Kudumu ya Bunge pia anaweza kuwasilisha muswada binafsi wa sheria na Waziri au Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiye anayeweza kuwasilisha muswada wa serikali bungeni.
Kanuni hizi zinafafanua kuwa miswada inaweza kuwa ya kawaida au ya dharura na kwamba, kuna utaratibu maalumu wa kuijadili na kuipitisha.
Ingawa Katiba inaeleza Bunge linatunga sheria, kwa mujibu wa kanuni za Bunge, inabainisha anayetunga miswada ya sheria ni Serikali.
Serikali ndiyo inayoandaa miswada na kuwasilisha bungeni kwa mjadala na marekebisho kabla ya kupitishwa kuwa sheria. Kwa mantiki hiyo, Bunge halitungi sheria moja kwa moja, bali linajadili, kurekebisha na kupitisha miswada iliyotayarishwa na Serikali.
Hili limejidhihirisha mara kadhaa pale ambako Bunge limepitisha sheria ambazo baadaye Mahakama Kuu imezitengua kwa kuwa ziko kinyume cha Katiba. Swali linalojitokeza ni:
Inawezekanaje Bunge lililojaa wanasheria mahiri likatunge sheria batili?
Jibu ni kwamba, sheria hizo batili hazijatungwa na Bunge moja kwa moja, bali na Serikali kupitia miswada yake.
Bunge kwa kuheshimu kanuni za uhusiano wa mihimili, hupokea miswada hiyo, kuijadili na kuipitisha.
Hata pale Mahakama inapobaini kasoro na kuitaka sheria husika ifanyiwe marekebisho, mara nyingi Bunge halichukui hatua, huku Serikali ikiendelea kupeleka miswada mingine yenye matatizo kama hayo.
Je, hali hii itaendelea mpaka lini?