Moshi. Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Camillus Wambura amesema jeshi hilo halitakubali mtu yeyote, kwa sababu yoyote, avuruge amani ya nchi kwa kisingizio cha harakati za uchaguzi.
IGP Wambura ameyasema hayo leo Ijumaa Machi 7, 2025, wakati wa kufunga mafunzo ya uongozi mdogo wa Jeshi la Polisi kwa ngazi ya Sajini na Koplo, katika Kambi ya Kilelepori Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro.
“Jeshi la Polisi tunatamka wazi kuwa hatutakubaliana na hatuko tayari kuona mtu yeyote anaivunja amani ya nchi hii na kusababisha vurugu au kufanya vitendo vyovyote viovu kwa kisingizio cha harakati za uchaguzi.
Lazima muda wote Watanzania na watu wote waishi kwa amani na usalama katika maeneo yao,” amesema IGP Wambura.
Amesema jukumu la kulinda amani lipo mikononi mwa askari wote nchini, wakiwemo wahitimu hao wa leo, ambao wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha usalama wa raia kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na rais utakaofanyia Oktoba 2025.
Aidha, amewataka wahitimu hao kuzingatia nidhamu, weledi na kuendelea kujifunza ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
“Hafla hii inanikumbusha maneno ya Biblia kutoka Mithali 4:13, ‘Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; mshike maana yeye ni uzima wako’. Hii inasisitiza umuhimu wa maarifa na mafunzo haya ambayo yamewaandaa si tu kwa kazi ya polisi bali pia kwa maisha yenu kwa ujumla,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Polisi Moshi, Ramadhani Mungi amesema mafunzo hayo yalifunguliwa Desemba 10, 2024, na kushirikisha wanafunzi 2,752, wakiwemo Sajini 1,820 na Koplo 932.

Baadhi ya askari wakionesha igizo la majukumu ya afisa wa polisi wakati wa uchaguzi
Amesema wanafunzi 23 waliondolewa kwa sababu ya utovu wa nidhamu na kushindwa kumudu mafunzo, huku wahitimu waliobaki wakijifunza uongozi, sheria, usimamizi wa haki za binadamu na utoaji wa huduma bora kwa jamii.
“Wahitimu hawa sasa wanarejea kwenye vituo vyao vya kazi wakitarajiwa kutumia maarifa waliyopata kuimarisha utendaji wa Jeshi la Polisi na kulinda usalama wa raia,” amesema SACP Mungi.
Kuhusu waliotimuliwa kwa utovu wa nidhamu, IGP Wambura ametaka wafuatiliwe nyendo zao kwani kama wameshindwa huko jeshini hata walipo wanaweza kuendeleza vitendo hivyo.
Katika hafla hiyo, baadhi ya askari walionesha igizo la majukumu ya ofisa wa polisi wakati wa uchaguzi hususan kabla na baada ya upigaji kura likisisitiza umuhimu la kila mmoja kufuata kanuni na sheria za uchaguzi.