Jumuiya ya nchi za pembe ya Afrika IGAD, inaonya kuwa mapigano yaliyoripotiwa siku chache nchini Sudan Kusini, na kukamatwa kwa washirika wa karibu wa Makamu wa kwanza wa rais Riek Machar, kunasukuma nchi hiyo kwenye uwezekano wa kutokea kwa vita vipya.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Onyo hili la IGAD, linakuja baada ya wakuu wa nchi hizo kukutana kwa njia ya mtandao siku ya Jumanne, na kutoa wito kwa pande zote kusitisha mzozo unaotishia kurejesha nchi hiyo kwenye vita.
Aidha, IGAD inataka kuachiwa huru kwa washirika wa Machar waliokamatwa kwa madai ya kushirikiana na waasi wanaofahamika kama White Army wanaodaiwa kuwa karibu na Machar na kutokea kabila lake la Nuer.
Waasi hao walishtumiwa kuvamia kambi ya jeshi katika mji wa Nasir tarehe nne mwezi huu.

Machar amekuwa akikanusha madai ya serikali kuhusika na kundi hilo, hatua ambayo ilishuhudia wanajeshi wakizingira makaazi yake jijini Juba wiki iliyopita.
Rais Salva Kiir licha ya mzozo huo, amesema kuwa Sudan Kusini haipo tayari kurejea kwenye vita, licha ya wachambuzi wa mambo wakisema iwapo sintofahamu hii haitasuluhishwa mkataba wa amani wa mwaka 2018, uliounda serikali ya muungano, huenda ukavunjika.
Jumamosi iliyopita, ubalozi wa Marekani iliwataka wafanyakazi wake wasiokuwa na kazi ya dharura kuondoka nchini humo kwa hofu kuwa, mzozo huo utaendelea, huku Uganda nayo ikiripotiwa kutuma vikosi vyake maalum jijini Juba, kuisadia serikali ya Sudan Kusini.