Idris Elba katika maisha ya Asake

Nigeria, Staa wa filamu duniani kutokea Uingereza, Idris Elba, 52, ameshiriki kuingiza sauti katika dokumentari inayosimulia maisha ya mkali wa Afrobeat kutokea Nigeria, Asake (30), ambaye anazidi kupanda chati.

Tangu ametoka kimuziki na albamu yake, Mr. Money with the Vibe (2022) na kushinda tuzo ya All Africa Music Awards (AFRIMA), umaarufu wa Asake umekuwa akikua kwa kasi kutokana na mfululizo wa nyimbo zake kali na albamu.

Na hivi karibuni amegonga vichwa vya habari kwa mara nyingine tena baada ya kuuza tiketi zote za onyesho lake la pili lililofanyika O2 Arena London nchini Uingereza, mafanikio hayo makubwa yanaonyesha jinsi amekuwa na mvuto kimataifa.

Mapema wiki hii kupitia ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 5, Asake alichapisha sehemu ya dokumentari hiyo ambayo inaonyesha safari yake ya muziki kutoka mwanzo wa hali ya chini hadi umaarufu katika sanaa.

Sauti ya Idris Elba mwenye asili ya Sierra Leone inasikika katika dokumentari hiyo yenye rangi nyeusi na nyeupe pekee ikisimulia mapambano ya Asake yalivyokuwa katika jiji lenye watu wengi la Lagos, Nigeria akitokea katika vitongoji duni.

Ikumbukwe Idris ambaye mwaka 2016 alitajwa na jarida la TIME katika orodha ya watu 100 wenye ushawishi mkubwa duniani, alishiriki katika filamu (biopic) kumuhusu Rais wa kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Mandela: Long Walk to Freedom (2013).

Miongoni mwa filamu maarufu alizocheza Idris ni pamoja na The Jungle Book, The Wire, Hobbs & Shaw, Beasts of No Nation, The Harder They Fall, Luther, The Suicide Squad, Star Treak Beyond, Beast n.k.

Hadi kufikia Mei 2019, filamu zake zilikuwa zimeingiza zaidi ya Dola 9.8 bilioni ikiwa ni pamoja na Dola 3.6 bilioni huko Amerika Kaskazini ambapo yeye ni miongoni mwa waigizaji wanaolipwa fedha nyingi.

Dokumentari hiyo ya Asake inakuja muda mfupi baada ya kuachia albamu yake ya tatu, Lungu Boy (2024) ikiwa na nyimbo 15 huku tisa kati ya hizo zikiingia katika chati ya Billboard U.S. Afrobeats Songs.  

Albamu hiyo iliyotoka chini ya rekodi lebo za YBNL Nation na Empire Distribution, imeshirikisha wasanii wakali kama Wizkid, Travis Scott, Stormzy, Central Cee na Ludmill huku watayarishaji wakiwa ni P.Priime, Magicsticks, Mike Dean, Sarz na Sak Pase.