Idadi ya watoto njiti yaongezeka Kanda ya Ziwa, wataalamu wataka utafiti

Idadi ya watoto njiti yaongezeka Kanda ya Ziwa, wataalamu wataka utafiti

Mwanza. Idadi ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda (njiti) imeendelea kuongezeka katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, hususan Mkoa wa Mwanza, hali inayowalazimu wataalamu wa afya kuomba ufanyike tafiti ili kubaini chanzo chake.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, zaidi ya njiti 120 wanapokelewa kila mwezi katika hospitali hizo mbili pekee.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Jesca Lebba, mkoa huo umepokea watoto 2,282 kwa mwaka 2024 kutoka watoto 1,789 mwaka 2019.

Huku, Wilaya ya Nyamagana yenye Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana na Sekou Toure ikiongoza kwa kupokea njiti 445 kwa mwaka 2019, mwaka 2020 watoto 478, 2021 watoto 459, mwaka 2022 ilipokea watoto 645, mwaka 2023 watoto 804 na mwaka 2024 ilipokea 983.

Mei 15, 2025 wakizungumza wakati wa kupokea msaada wa vibebeo maalumu kwa ajili ya huduma ya kangaroo (ngozi kwa ngozi) vilivyotolewa na Kampuni ya Babymoon ikiwa ni maadhimisho ya siku ya huduma hiyo duniani, Mkuu wa Idara ya Watoto Hospitali ya Sekou Toure, Dk Magreth Guranywa alisema hospitali hiyo hupokea kati ya watoto njiti 70 hadi 90 kwa mwezi.

“Tumepata wimbi kubwa la watoto njiti katika miaka ya karibuni, kama tunavyojua watoto njiti ni wanaozaliwa kabla ya muda wa wiki 37. Sisi tunaendelea kupambana kwa kuwatunza, kuwahudumia na kuwatibu kwa sababu, ni sehemu ya watoto ambao ni wagonjwa, tunaowapokea katika hospitali yetu.

“Tunapokea watoto kati ya 150 hadi 200 kwa mwezi wenye changamoto mbalimbali, lakini kundi kubwa tunapata la watoto njiti ambao ni kati ya 70 hadi 90 kwa mwezi, kwa hiyo ni idadi kubwa kidogo. Na wakati wa kuchukua historia kuwa ni kitu gani kinasababisha watoto njiti, tatizo limekuwa likionekana ni maradhi mbalimbali, ikiwemo presha wakati wa ujauzito au maambukizi kupitia via vya uzazi,” anasema Dk Guranywa.

Anasema kwa sasa njia inayoweza kusaidia tatizo hilo ni wanawake kuwahi kliniki mara tu wanapobaini ni wajawazito, kwa kuwa wanapowahi kliniki inawawezesha wahudumu wa afya kufuatilia maendeleo yao na watoto waliopo tumboni.

Muuguzi Kiongozi wa kitengo cha watoto Bugando, Dismas Mauki amesema hospitali hiyo ambayo awali ilikuwa inapokea njiti mara moja moja, sasa inapokea watoto hao kila siku na kufanya idadi yao kwa mwezi kufikia kati ya 30 hadi 40 wakitokea mikoa ya Kanda ya Ziwa, hususani mkoani Mwanza.

“Zaidi wanaotoka Mkoa wa Mwanza, kwa wastani tunaweza kupokea watoto 30 hadi 40 kwa mwezi na tunapokea watoto hadi wenye gramu 800 ambao wanaingia kwanza ICU (chumba cha uangalizi maalumu), yanaendelea madawa wakimaliza dawa zao  na uzito ukiongezeka ndio tunawapeleka kangaroo.

 “Sasa hivi tuna ongezeko la watoto hapa  Bugando kwa sababu zamani tulikuwa tuna ruka hata siku moja, tunaweza tukawa na mtoto mmoja na siku nyingine inaruka, tunaweza kumaliza hata siku tatu hatujapata, lakini kwa sasa hakuna siku ambayo inapita hatujapokea mtoto ambaye ni njiti.”

Ameishukuru kampuni hiyo kwa kutoa vibebeo, akieleza kuwa ni moja ya mahitaji ya kuwahudumia watoto njiti, ambavyo vitawasaidia mama zao kuwaweka vifuani kati ya saa nane hadi 24, kama inavyoelekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), ili wapate joto na kuongezeka uzito.

Mama aliyejifungua mtoto njiti, Rosemary Kusekwa anasema kilichosababisha apate mtoto huyo ni baada ya kuanza kutoka maji kwenye viungo vya uzazi,  ambayo wakati wa mahudhurio ya kliniki alielezwa ni dalili ya hatari kwa mjamzito.

Anasema baada ya kuyaona alienda hospitalini kwa uchunguzi ambapo alifanyiwa vipimo, kikiwemo cha ultrasound kisha akaambiwa maji yamepungua.

“Kupungua kwa maji hayo ilikuwa ni changamoto kwa mtoto, hivyo wakanishauri niendelee kukaa hapo kwa ajili ya uangalizi ambapo nilikaa kwa kipindi cha wiki moja baadaye nikarejea nyumbani.

“Baada ya siku mbili hali ikawa tofauti, maji yakaendelea kutoka na kuhisi tumbo la chini linauma sana, ndipo nikapelekwa Sekou-Toure … madaktari walinieleza njia imefunguka na mtoto yupo tayari kutoka,” amesema Kusekwa.

Amesema ndipo alijifungua mtoto njiti akiwa na umri wa miezi sita na wiki mbili, sasa hivi ana miezi 6 na wiki tatu akieleza kuwa kulea mtoto njiti ni changamoto kwa sababu anahitaji uangalizi mkubwa na umakini wa kumpatia dawa anazozitumia.

“Pia unyonyeshaji kila baada ya saa 3 mtoto anatakiwa kupata maziwa ambayo nayo ni kwa kipimo elekezi,” anaeleza.

Lusia John, aliyekuwa na siku sita tangu ajifungue, anasema uangalizi wa mtoto huyo ni muhimu kuliko chochote na iketokea akakosea maelekezo anaweza kumpoteza.

“Nashukuru kupata bebeo kwa sababu limenirahisishia kumbeba mtoto, mwanzoni nilikuwa napata changamoto ya kumfunga, mpaka nisubiri mtu kumuomba msaada kunifunga, lakini kwa sasa naweza kujifunga mwenyewe na nikawa sawa kuliko kanga nilizokuwa natumia. Wakati wote nilikuwa nahisi kumuangusha mtoto wangu,” anasema.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Babymoon, Albany James ameahidi kushirikiana na hospitali hizo kufanya tafiti ili kubaini sababu za ongezeko la watoto hao Kanda ya Ziwa.

“Tunakuahidi kuwa kadri ambavyo tutakuwepo hapa tutasaidia kwenye huo utafiti wa kutaka kujua kwa nini kuna ongezeko kubwa ukanda huu, tuna rasilimali, tuna watu kwa ajili ya kuhakikisha haya yote yanakwenda vizuri,” amesema.

Anasema pamoja na kutoa vibebeo hivyo, pia wanatatoa elimu kwa wanawake wenye watoto hao namna ya kuvitumia kwa kuwa ni rahisi kuliko kufunga kanga na taulo ambazo zinachosha, hasa maeneo yanayofungwa fundo, na hazitoi nafasi kwa mama kujishughulisha na kazi zingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *