Idadi ya waliofariki yapindukia 200 katika mji wa Sudan ulioko kwenye mzingiro wa RSF

Idadi ya watu waliopoteza maisha katika mji wa Al-Hilaliya wa katikati mwa jimbo la Al Jazirah nchini Sudan, imeongezeka na kufikia zaidi ya 200 kufuatia wiki mbili za mzingiro na mashambulizi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF.

Kwa mujibu wa taarifa ya Muungano wa Madaktari wa Sudan, RSF iliongeza mashambulizi yake katika mji huo kuanzia Oktoba 25 na idadi hiyo ya watu waliopoteza maisha ni pamoja na wale waliokufa kutokana na ugonjwa, njaa na mateso.

Muungano huo umeripoti kuweko uhaba mkubwa wa huduma za afya kutokana na kuzingirwa mji huo ikibainisha kuwa wakazi wengi wamelazimika kunywa maji yasiyo salama na hivyo kukumbwa na magonjwa ya miripuko.

Taarifa ya muungano huo ambayo bado haijajibiwa na RSF pia imesema: “Vikosi vya RSF vinawashikilia wakazi wa mji huo katika misikiti kadhaa na haviwaruhusu kuondoka isipokuwa walipe kiasi kikubwa cha pesa.”

Tangu katikati ya Aprili 2023, Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan SAF na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF vinapigana katika vita angamizi vya uchu wa madaraka na vimeshasababisha vifo vya zaidi ya Wasudan 20,000 na zaidi ya milioni 10 wengine kukimbia makazi yao. 

Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa yanahimiza kumalizwa vita hivyo kwani vimewasukuma mamilioni ya Wasudan kwenye ukingo wa njaa na vifo kutokana na uhaba wa chakula, huku mapigano yakiendelea katika majimbo 13 kati ya 18 ya Sudan.