
Idadi ya vifo vilivyotokana na mripuko wa lori la petroli wiki iliyopita katika jimbo la Jigawa la kaskazini mwa Nigeria imeongezeka na kufikia watu 181.
Gavana wa jimbo hilo Umar Namadi amewaambia waandishi wa habari kwamba zaidi ya watu 80 wamelazwa hospitalini baada ya dereva wa lori la mafuta ya petroli kushindwa kulidhibiti na kupinduka katika mji wa Majiya ulioko katika eneo la serikali ya mtaa wa Taura, usiku wa Oktoba 15.
Alisema familia 210 ziliathiriwa na mripuko huo na wengi wa wahanga hao ni watu waliokimbilia eneo la tukio kuchukua petroli iliyomwagika kwenye mtaro wa maji baada ya lori hilo kupinduka.
Alibainisha kuwa, serikali ya jimbo hilo ilikuwa imelipa bili za matibabu ya wahanga wote na inajitahidi kuhakikisha kuwa familia zilizoathiriwa na mripuko huo zinaendelea na maisha yao.
Mazishi makubwa ya wahanga wa ajali hiyo yalifanyika Oktoba 16 katika mji huo Majiya lakini tangu wakati huo hadi hivi sasa idadi ya wahanga hao inazidi kuongezeka kutokana na majeruhi mabaya waliyopata baadhi ya watu.