Idadi ya fedha, wadai wa mwigizaji Nicole waongezeka

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema kiwango cha fedha na idadi ya wanaodai kudhulumiwa na mwigizaji Joy Mbaga, maarufu Nicole Berry, imeongezeka.

Nicole anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay, Kinondoni tangu Machi 3, 2025 akituhumiwa kwa udanganyifu, ikielezwa amekuwa akiendesha upatu kwa njia ya mtandao wa kijamii.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 7, 2025 Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema idadi ya waliojitokeza kulalamika juu ya mtuhumiwa kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu kutoka kwao imeongezeka.

“Watu kadhaa wameendelea kujitokeza kulalamika juu ya mtuhumiwa alivyojipatia pesa kwa udanganyifu, lakini suala la mahakamani Jeshi la Polisi kama ilivyo desturi ya kisheria tutamfikisha haraka iwezekanavyo,” amesema Kamanda Muliro.

Nicole, ambaye pia ni mfanyabiashara anatuhumiwa kujipatia zaidi ya Sh100 milioni kwa udanganyifu.

Akizungumza na Mwananchi Machi 5, 2025, Kamanda Muliro alisema Nicole (32) alikamatwa Machi 3, 2025, akielekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ajili ya kusafiri kwenda Lagos, Nigeria.

“Anatuhumiwa kujipatia pesa kwa njia mbalimbali za udanganyifu kwa kutengeneza magrupu ya upatu kwenye mitandao kinyume cha sheria. Anatengeneza watu wa uongo katika magrupu hayo ili kuwavuta wengine.

“Wakati mwingine, wakiweka laki moja baada ya mzunguko, anawaonyesha watu 48 ambapo unaweza kuwa wa kwanza, wa tatu au wa 10 kupokea,” alisema na kuongeza;

“Ukifanya hesabu, unaona baada ya muda mfupi unaweza kupata kama milioni nne na kitu. Anatengeneza magrupu mengi, watu wanachangia, lakini ni magrupu ya uongo. Wewe unayeingia, ndiyo unakuwa unatapeliwa.”

Alisema tayari walikuwapo walalamikaji zaidi ya 18 waliokwenda kuripoti Kituo cha Polisi Oysterbay.

Katika hatua nyingine, amesema polisi kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kisheria, ikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wamewakamata watuhumiwa 25 wanaojihusisha na makosa ya kimtandao katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na mikoa mingine.

Amesema wanatuhumiwa kuongoza kikundi cha kihalifu mtandaoni, kutumia laini za simu zisizo na usajili wao, kuingilia na kubadili namba za utambuzi halisi wa simu (IMEI), kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu na kujifanya maofisa wa mfuko wa pensheni na kuwaibia wastaafu na kutenda makosa ya utakatishaji wa fedha.

Amesema watuhumiwa hao ni pamoja na Kelvin Sauro mkazi wa Ifakara na wenzake 14.

“Watuhumiwa wamekuwa wakituma ujumbe kama tuma ile hela kwa namba hii, tuma kwenye namba hii ile pesa ya kodi. Leta namba za Nida, vitambulisho tukushughulikie mapunjo yako ya kustaafu,” amesema Kamanda Muliro.

Amesema pia Enrigue Adolph Ngagani na wenzake wanne wa Sinza, Dar es Salaam wanashikiliwa kwa tuhuma za kumiliki akaunti za mtandao wa Tiktok zinazotumika kusambaza taarifa zenye maudhui ya udhalilishaji wa watu kupitia programu za akili mnemba (Al)

Kamanda Muliro amesema mtuhumiwa mwingine anayeshikiliwa ni Baruani Majani, mkazi wa Kahororo mkoani Kagera na wenzake wanne wakidaiwa kufanya  udanganyifu kwa wastaafu na kuwaibia pesa kwa kujifanya kuwa ni wafanyakazi wa mfuko wa pensheni hivyo  wanashughulika na mapunjo ya wastaafu.

Baadhi ya watuhumiwa, amesema wamekamatwa wakiwa na vifaa vya kielektroniki zikiwamo simu janja 10, simu za kawaida 26, laini za simu 84 za kampuni mbalimbali, memory card mbili, kompyuta mpakato moja, mashine mbili za kusajili laini, gari na funguo moja ambalo ni mazalia ya uhalifu wao.

Amesema baadhi ya watuhumiwa wamefikishwa katika Mahakama Ya Hakimu Mkazi Kisutu na wengine taratibu za kisheria zinakamilishwa ili wafikishwe mahakamani.

Ametoa wito kwa wananchi kufuata sheria na kanuni za matumizi ya mitandao, akiwatahadharisha kutokutoa vitambulisho kama vile vya Nida kwa watu wasiowajua.

“Polisi inatoa onyo kali dhidi ya wote wanaojihusisha na makosa ya kimtandao na mengine, kwani watu hao watashughulikiwa vikali lakini kwa mujibu wa sheria,” amesema.