
Mwakilishi wa Palestina ameiambia Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) siku ya Jumatatu kuwa Israeli ilikuwa ikitumia kuzuia misaada ya kibinadamu kama “silaha ya vita” huko Gaza, huku wiki moja ya vikao vya kusikilizwa vikianza mjini Hague kuhusu wajibu wa kibinadamu wa Israeli kwa Wapalestina.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Israeli, ambayo haishiriki katika vikao, mara moja imejibu, ikilaani “mateso ya utaratibu.”
Mahakama ya ICJ, iliyoko Hague, nchini Uholanzi, imefungua wiki yake ya kusikilizwa kwa kesi zaidi ya siku 50 baada ya kuanzishwa kwa kizuizi kamili cha misaada inayoingia Ukanda wa Gaza ulioharibiwa na vita.
“Maduka yote ya kuoka mikate yanayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa huko Gaza yamelazimika kufungwa. Tisa kati ya Wapalestina kumi hawana maji safi,” Ammar Hijazi, mwakilishi wa Palestina katika mashirika ya kimataifa, amesema siku ya Jumatatu katika ufunguzi wa kikao hicho.
“Majengo ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa yako tupu… Njaa imekita mizizi hapa. Misaada ya kibinadamu inatumika kama silaha ya vita,” ameongeza mbele ya jopo la majaji 15.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Israeli Gideon Saar, akizungumza mjini Jerusalem, utaratibu huo “ni sehemu ya mateso ya kimfumo na uhalalishaji wa kimfumo wa Israeli.”
“Sio Israeli ambayo inapaswa kuhukumiwa. Ni UN na UNRWA” (shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina), amewaambia waandishi wa habari.
Israeli ilipitisha sheria ya kupiga marufuku shirika tanzu la Umoja wa Mataifa kufanya kazi katika ardhi ya Israeli baada ya kuwashutumu baadhi ya wafanyakazi kwa kuhusika katika shambulio la vuguvugu la waislamu wa Palestina Hamas tarehe 7 Oktoba 2023, ambalo lilizusha mzozo huo.
Uchunguzi huru unaonyesha kuwa Israeli haijatoa ushahidi kuhusiana na madai haya.
Mwezi Desemba, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuitaka ICJ kutoa maoni ya ushauri “kama jambo la kipaumbele na la dharura.”
Azimio hilo linaitaka ICJ kufafanua wajibu wa Israeli kuhusu uwepo wa Umoja wa Mataifa, mashirika yake, mashirika ya kimataifa, au mataifa ya tatu ili “kuhakikisha na kuwezesha utoaji wa haraka wa mahitaji muhimu kwa maisha ya raia wa Palestina.”
Israeli inadhibiti mtiririko wote wa misaada ya kimataifa, muhimu kwa Wapalestina milioni 2.4 katika Ukanda wa Gaza, ambao wanakabiliwa na janga la kibinadamu ambalo halijawahi kushuhudiwa, na kuwakatilia mbali Machi 2, siku chache kabla ya usitishaji vita dhaifu kuporomoka baada ya miezi 15 ya mapigano yasiyokoma.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, takriban Wapalestina 500,000 wameyakimbia makazi yao tangu kumalizika kwa usitishaji vita uliodumu kwa miezi miwili.
Israeli ilianza tena mashambulizi yake ya anga na ardhini mnamo Machi 18, na kuua Wapalestina wasiopungua 2,111 na kusababisha kile ambacho Umoja wa Mataifa ulikieleza kuwa “huenda mgogoro mbaya zaidi” wa kibinadamu katika eneo hilo tangu kuanza kwa vita.