
Libya imekubali mamlaka ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita uliofanywa nchini humo, licha ya kutokuwa sehemu ya Mkataba wa Roma, mkataba unaoanzisha mahakama hiyo, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC Karim Khan amesema siku ya Alhamisi.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Ninakaribisha kwa moyo mkunjufu ujasiri, uongozi na uamuzi wa mamlaka ya Libya,” Khan ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akisisitiza kwamba uamuzi huu “unawakilisha hatua muhimu kuelekea jukwaa jipya la hatua za pamoja.”
Serikali ya umoja wa kitaifa yenye makao yake makuu mjini Tripoli imekubali kuipa mahakama mamlaka juu ya madai ya uhalifu wa kivita na ukandamizaji ulioanza wakati wa uasi wa mwaka 2011 ambao ulimuua dikteta Muammar Gaddafi na miaka kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyofuata, Khan ameongeza.
Mamlaka ya ICC itarefushwa hadi mwisho wa mwaka 2027. Mahakama hiyo imepewa mamlaka na Baraza la Usalama tangu mwezi Februari 2011.
Pamoja na mapigano yakiwa yamezuka tena mjini Tripoli wiki hii, Libya imekabiliwa na hali ya kutokuwa na utulivu tangu uasi wa mwaka 2011,ulioungwa mkono na NATO uliomuangusha Gaddafi, kiongozi mkandamizaji wa Libya aliyetawala tangu mwaka 1979.
Nchi hiyo imesalia kugawanyika kati ya serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli, inayoongozwa na Waziri Mkuu Abdulhamid Dbeibah, na serikali pinzani ya mashariki, inayodhibitiwa na familia ya Haftar.
Khan pia ametoa wito kwa Mwanasheria Mkuu wa Libya Al-Seddik al-Sour kumkamata Osama Almasri Najim – ambaye yuko chini ya hati ya kukamatwa iliyotolewa na ICC mwezi Januari – “na kumkabidhi kwa ICC.”
Najim anatafutwa kwa mauaji, ubakaji, unyanyasaji wa kingono na utesaji, uliofanywa tangu mwaka 2015 alipokuwa akisimamia kituo cha Mitiga huko Tripoli. Matendo yake mara nyingi yalichochewa na madai ya uhalifu dhidi ya dini, kama vile “tabia mbaya.”
Alikamatwa mjini Turin, kaskazini mwa Italia, Januari 19, kwa kibali cha ICC, aliachiliwa kwa misingi ya kiutaratibu na kurejeshwa Tripoli, mji mkuu wa Libya, siku mbili baadaye akiwa ndani ya ndege ya Jeshi la Wanahewa la Italia.
Khan amesema uchunguzi huo utachunguza kwa kina vituo vya kizuizini vya Libya, ambavyo aliviita “sanduku jeusi la mateso kwenye pwani ya Mediterania ambalo hakuna mtu alitaka kufungua.”
Khan pia ameahidi kuwachukulia hatua kali viongozi wa wanamgambo ambao amesema bila shaka wanahisi “ufahamu unaokua wa utawala wa sheria unaoingia katika ardhi ya Libya.”