
Katika historia ya Tanzania, jina la Profesa Philemoni Sarungi (89) ni miongoni mwa majina ya Watanzania wachache waliokuwa viongozi na wataalamu waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
Alikuwa daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa na waziri wa zamani wa Serikali, ambaye ameaga dunia Machi 5, mwaka huu. Kutokana na tukio hilo, Tanzania inaomboleza kifo chake.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Msemaji wa familia ya Chifu Sarungi, Martin Sarungi, ilisomeka hivi: “Familia ya Chifu Sarungi na ukoo wa Nyiratho wa Utegi, Rorya tunasikitika kutangaza kifo cha mpendwa wetu Mzee Profesa Philemon Mikol Sarungi kilichotokea leo Machi 5,2024 saa kumi jioni.”
Martin alisema Profesa Sarungi siku chache zilizopita alikuwa akisumbuliwa na malaria lakini alipona. “Mzee kama unavyojua alikuwa tayari ana umri mkubwa na siku chache zilizopita alisumbuliwa na malaria lakini alipata nafuu,” amesema.
Martin alisema shughuli za mazishi zinasubiri watoto na wajukuu zake ambao wengi wanaishi nje ya nchi na mwili umehifadhiwa Hospitali ya Lugalo.
Awali taarifa ya kifo cha Profesa Sarungi ilitangazwa na binti yake Maria Sarungi ambaye kwenye ukurasa wake wa X aliweka picha ya baba yake na kuandika “Rest with Angels, Daddy”.
Mikol Philemon Sarungi alizaliwa Machi 23, 1936 huko Tarime, mkoani Mara, wazazi wake wakiwa Sarungi Igogo Yusufu na Amimo (Maria) Sarungi. Safari ya kielimu ya Profesa Sarungi ilianza kwa ari na bidii, na baadaye alijitosa katika masomo ya tiba nje ya nchi.
Mwaka 1966 alihitimu Shahada ya Udaktari wa Tiba (Doctor of Medicine) kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Szeged, Hungary.
Miaka minne baadaye, mwaka 1970, alipata Shahada ya Uzamili katika Upasuaji (Master in Surgery) kutoka chuo hichohicho.
Mwaka 1973 alihitimu Diploma katika Orthopedics/trauma kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Vienna na mwaka 1975 alipata Diploma ya Upasuaji wa Replantation Surgery kutoka Chuo Kikuu cha Shanghai, China.
Baada ya kurejea Tanzania, Profesa Sarungi alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1971 kama mhadhiri na katika idara ya upasuaji. Alipanda vyeo hadi kuwa Mkuu wa Idara ya Upasuaji na baadaye kuwa Profesa kamili.
Safari ya kitaaluma
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Sarungi alikuwa mhadhiri wa upasuaji (1971-1973), Mhadhiri Mwandamizi (1973-1976), Profesa Mshiriki (1977-1979) na Mkuu wa Idara ya Upasuaji (1977-1984).
Mwaka 1979 aliteuliwa kuwa Profesa kamili wa upasuaji. Baadaye akawa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Tiba cha Muhimbili (1984-1990), Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1989-1991) na 1985 – Kiongozi wa Idara ya Tiba ya Mifupa katika Kitivo cha Tiba.
Mwaka 1990, Profesa Sarungi alisema katika mkutano wa chama cha madaktari kuwa “kuwazuia madaktari wa sekta ya umma kufanya kazi binafsi ni kuwalazimisha kuelekeza nguvu zao na taaluma mahali pengine”.
Safari ya kisiasa
Mchango wa Profesa Sarungi haukuishia katika taaluma ya tiba pekee. Alijitosa katika siasa na kuhudumu kama Mbunge wa Jimbo la Rorya kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Miongoni mwa nyadhifa mbalimbali za uwaziri alizoshika ni pamoja na Waziri wa Afya, Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi , Waziri wa Elimu na Utamaduni, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Kitabu kinachoitwa ‘The Making of a Nation: What Makes People RICH and Nations POWERFUL’, kilichoandikwa na Festo Michael Kambarangwe, kinamtaja Profesa Sarungi kama mfano wa watu waliotoa mchango mkubwa kitaaluma lakini wakaelekezwa katika siasa.
Kitabu hiki kinaeleza: “Mzungumzie Profesa Sarungi, mtu aliyeng’ara katika elimu na taaluma yake kama daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa wa kiwango cha juu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Je, alihudumu kwa muda mrefu katika sayansi ya mifupa? Hapana! Alihudumu Tanzania kama waziri wa vifaa vya kijeshi? Nilisema waziri wa vifaa? Haina tofauti—alikuwa Waziri wa Ulinzi.”
Maneno haya yanaonyesha changamoto ambazo wataalamu wanakutana nazo katika kubaki kwenye taaluma zao kutokana na vipaumbele vya kitaifa, na hivyo kulazimika kuingia katika siasa.
Mchango katika michezo
Profesa Sarungi alikuwa mpenzi na mwanachama wa klabu ya Simba SC. Alitoa mchango mkubwa katika klabu hiyo, hasa katika kusaidia wachezaji kupata matibabu. Mbali na siasa, pia alikuwa mpenda michezo kama yoga, kukimbia na mazoezi ya viungo. Mwaka 2021, alitunukiwa Tuzo ya Heshima na klabu ya Simba SC kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya timu hiyo.
Kwa mujibu wa gazeti dada la Mwananchi, Mwanaspoti, Aprili 2021 uongozi wa klabu ya Simba ulipanga kumpa Profesa Sarungi tuzo ya Heshima kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya timu hiyo.
Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo Ijumaa, Aprili 9, 2021 ilieleza kwamba Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Mohammed Dewji, alimchagua Sarungi kuwa mshindi wa kipengele hicho ambacho kinalenga kuwakumbuka na kuthamini wale waliotoa mchango ndani ya klabu hiyo miaka ya nyuma.
“Kwa kutambua mchango wake ndani ya Simba, Mwenyekiti wa Bodi, Mohammed Dewji amemchagua Profesa Philemon Sarungi kuwa mshindi Tuzo ya Heshima (Lifetime Achievement) ambayo itatolewa kwenye hafla ya Tuzo za Mo Simba 2021 ambazo zitafanyika mwishoni mwa msimu.
Urithi na mwisho wa safari
Profesa Sarungi aliandika kitabu kiitwacho “Historia ya Uzawa wa Rumbasi (Wategi)”, ambacho alikikabidhi kwa Maktaba ya Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni ili kusaidia Watanzania kufahamu na kujivunia historia yao.