Marekani. Mwaka 1994 ndipo The Notorious B.I.G aligundua kipaji cha Lil’ Kim na kumkaribisha katika kundi lake, Junior M.A.F.I.A na ukawa mwanzo wa mafanikio ya Rapa huyo na mengine sasa ni historia, huku awali akivutiwa na kina MC Lyte na Lady of Rage.

Albamu ya kwanza ya Lil’ Kim, Hard Core (1996) ilifanya vizuri na hadi sasa imeuza nakala zaidi ya milioni sita duniani kote na kutoa nyimbo kali kama No Time, Not Tonight (Ladies Night), Crush on You n.k.
Zilifuata albamu nyingine kama The Notorious K.I.M. (2000), La Bella Mafia (2003) na The Naked Truth (2005), hizo zilitosha kumfanya kuwa msanii mkubwa duniani na baada ya miaka 14 akaachia albamu yake ya mwisho, 9 (2019).
Mwaka 2001 Lil’ Kim aliionja namba moja ya chati za Billboard Hot 100 kupitia wimbo wake, Lady Marmalade ulioshinda Grammy (2002) na kumfanya kuwa mmoja wa wasanii wachache wa kike wa Rapa kuwa na namba moja kwenye chati hizo.

Kufika mwaka 2005 Lil’ Kim alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kusema uwongo mbele ya mahakama kuhusu kuhusika kwake katika tukio la ufyatulianaji risasi na marafiki zake miaka minne iliyopita.
Baadaye zilifuata mfululizo wa makala, Lil’ Kim: Countdown to Lockdown kuhusu kifungo chake zilizorushwa kwa mara ya kwanza BET mwaka 2006, kisha akatoa mixtape yake ya kwanza, Ms. G.O.A.T. (2008).

Miaka ya 2010 Lil’ Kim aliendelea kushirikiana na wasanii kama Faith Evans, Remy Ma, Fabolous n.k, na ndicho kipindi alikuja Tanzania kwa ajili ya Fiesta na kufanya show ambayo imeacha historia kwa mashabiki na hata wasanii akiwemo Juma Nature aliyetumbuiza naye.
Katika show hiyo iliyofanyika Leaders Club, ni kama mashabiki wa Bongo hawakumuelewa sana Lil’ Kim, hivyo akatafutwa msanii mwenyeji ambaye anaweza kushirikiana naye, ndipo Nature akachukua nafasi hiyo na kuokoa jahazi.
Kwa mujibu wa Nature alikuwa anafahamu nyimbo chache za Lil’ Kim alizoshirikiana na Notorious B.I.G mwishoni mwa miaka ya 1990, hata Kim alikuwa haujui muziki wa Nature ili walifanya kitu wakitumbuiza pamoja ngoma ya Nature, Hakuna Kulala (2005).