Huyu ndiye Dk Albina Chuwa, Mkurugenzi mstaafu wa NBS

Dodoma. Dk Albina Chuwa si jina geni miongoni mwa Watanzania kutokana na kusimamia sensa ya watu na makazi mara mbili mfululizo akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Mtakwimu Mkuu wa Serikali.

Dk Chuwa, ambaye ameishika nafasi hiyo kwa miaka 17 tangu mwaka 2007, licha ya kustaafu, aliongezewa muda kwa vipindi viwili kuendelea na nafasi hiyo hadi Februari 13, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya uteuzi wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali mwingine, Dk Amina Msengwa.

Ndani ya kipindi alichohudumu katika ofisi hiyo, Dk Chuwa amesimamia sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 na ile iliyofanyika kwa mara ya kwanza kidijitali mwaka 2022.

Dk Chuwa anasema alisoma masomo ya sayansi tangu sekondari, na baada ya kumaliza chuo kikuu, mwaka 1986 aliajiriwa na NBS. Mwaka 2007 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NBS na Mtakwimu Mkuu wa Serikali.

Aliyekuwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk Albina Chuwa (kushoto) akimkabidhi hati ya makabidhiano Mtakwimu Mkuu mpya wa Serikali Dk Amina Msengwa kwenye hafla ya makabidhiano iliyofanyika Takwimu House Dodoma.  Dk Msengwa aliteuliwa na kushika wadhifa huo Februari 23, 2025.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi wiki iliyopita nyumbani kwake jijini Dodoma, Dk Chuwa anasema kwa mara ya kwanza alipelekewa barua ya kuteuliwa kuwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali ofisini jijini Dar es Salaam, ambapo mhudumu alimpelekea barua hiyo kutoka Wizara ya Fedha na Mipango.

Anasema baada ya kuipokea barua na kujua ni ya uteuzi huo, alipiga magoti na kumshukuru Mungu na kumuomba amuongoze katika majukumu yake.

Anasema alifanya hivyo kwa kuwa aliona jukumu alilopewa ni kubwa kwake, kwa sababu wakati huo suala la takwimu halikuwa kitu kinachoeleweka kwa viongozi wengi barani Afrika na wananchi kwa ujumla.

“Jambo hilo lilinifanya kuwaza, naanzia wapi suala hili la takwimu lieleweke na kutumika ndani ya Bara la Afrika? Lakini kwa msaada wa Rais Kikwete (Rais wa awamu ya nne) na viongozi wengi, liliwezekana,” anasema.

Anasema alipoingia ofisini, jambo la kwanza alilolifanya ni kuhakikisha wafanyakazi wanajengewa uwezo baada ya kukuta ni watakwimu watatu pekee, ndio waliokuwa na shahada ya pili.

“Pia kulikuwa hakuna mpango kabambe wa kuimarisha takwimu nchini, huwezi kuongoza bila kuwa na mpango kabambe wa Taifa wa kuongoza takwimu na kuratibu masuala ya takwimu. Nilichofanya ni kushirikiana na wadau, ambao ni Benki ya Dunia, tukaanzisha mpango wa kuboresha na kuimarisha takwimu nchini,” anasema Dk Chuwa, na kuongeza:

“Suala la takwimu ni gumu, sio kitu cha urahisi sana. Kwa hiyo kuwapeleka watu wakasome halafu wakasafiri nje ya nchi na kuona watu wanafanyeje, hilo lilisaidia kubadilisha fikra zao. Serikali na viongozi wakiwemo mheshimiwa Rais walinisaidia sana, na wananchi pia walinipa ushirikiano mkubwa,” anasema.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dk Albina Chuwa.

Akizungumzia nguvu kazi aliyoikuta ofisini, Dk Chuwa anasema kulikuwa na idadi ndogo ya wanawake, jambo lililoweka ugumu kwake kukubalika na wafanyakazi, hivyo ilimlazimu kufanya kazi ya ziada huku akiwashauri wanawake na wasichana kupenda hesabu kwa sababu sio masuala magumu, wanaweza wakitia bidii.

Kwa nini takwimu?

Dk Chuwa anasema takwimu ni muhimu kwa sababu ni ngumu kupanga mipango ya maendeleo bila kuwa na takwimu, na zinabeba mchango wa asilimia 100 katika maendeleo ya makundi yote.

“Mfano, Bara la Afrika lenye watu bilioni 1.7, tunaendaje kupanga mipango ya maendeleo kama hatujui watu hao wanaishije, hali za umaskini ikoje, na tunakwenda kusaidiaje?” anahoji.

Anasema ni ngumu kupanga mipango yoyote bila kuwa na takwimu, hivyo kumshauri Mtakwimu Mkuu mpya kuhakikisha wanazalisha takwimu nyingi ambazo zipo kwenye lugha nyepesi.

Alichobaini kupitia takwimu

Dk Chuwa anasema katika sensa ya mwaka 2022, wamebaini kuwa asilimia 24 ya wanawake wote wenye umri wa miaka 14 na kuendelea ndio wanaomiliki ardhi, nyumba, na vitu vyenye thamani.

“Ningetamani kuona asilimia 50 hata 70 ya wanawake nasi tunamiliki hivi vitu, kwa sababu Serikali yetu inatoa kipaumbele kwa makundi yote. Hii takwimu haijanifurahisha, lakini juhudi zinazofanywa na Rais na Serikali, nina imani tutakapofanya sensa nyingine mwaka 2032 takwimu itapanda,” anasema.

Pia, anasema katika utafiti wa mapato na matumizi ya kaya, wamebaini kaya asilimia 36 kati ya takribani milioni 14 zilizopo nchini, zinaongozwa na wanawake, ambao wanapambana kwa kiasi kikubwa kiuchumi.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dk Albina Chuwa.

Dk Chuwa, ambaye pia anashika nafasi mbalimbali duniani katika taaluma yake ya takwimu, anasema kwenye uchambuzi wa takwimu hizo inaonyesha vyanzo vya maji vimeboreshwa zaidi katika kaya zinazoongozwa na wanawake.

Mbali na hilo, anasema watoto wanaotokana na kaya hizo zinazoongozwa na wanawake wengi wanakwenda shuleni, hasa katika kaya zilizoko Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

Anasema mchango wa takwimu pia unaonekana kwa kuonyesha umiliki wa wanawake katika vitu visivyohamishika, bado unahitajika kwa kuongeza idadi yao, hivyo inahitajika kuongeza nguvu zaidi angalau kufikia asilimia 50 au 70.

Ushiriki wa wanawake

Ili kuongeza ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi na hesabu, Dk Chuwa anasema Serikali iendelee na jitihada inazofanya za kutoa miongozo mbalimbali.

Hata hivyo, anashauri wakati jitihada hizo zinafanyika za kuongeza ushiriki wa wanawake na wasichana, wavulana na wanaume wasisahaulike, ingawa msukumo unatakiwa kuwa kwa wasichana na wanawake zaidi.

Anasema pia jumuiya za watu kwenye ngazi za chini na wazazi wana jukumu la kuongeza ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi na takwimu kwa kuwahamasisha na kuwafundisha wakiwa katika ngazi za chini.

“Serikali imeshaweka jitihada kwa kuboresha mitaala kwenye masomo ya sayansi, teknolojia na ubunifu. Tunaona mabadiliko makubwa sasa, watoto wa kike ndio wanaongoza ukilinganisha na enzi zetu ambapo wanaume ndio walikuwa wanaongoza,” anasema.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akiwa na aliyekuwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa, Katika Ofisi ya Waziri wa Fedha, Treasury Square, Jijini Dodoma.

Dk Chuwa anasema dunia inakwenda kwenye matumizi ya akili mnemba (AI), hivyo hakuna namna ya kufanya ila kupambana kwa kubadilisha fikra kwa kwenda sambamba na masomo ya sayansi.

Hata hivyo, anasema wakati mkazo unatiliwa katika masomo ya sayansi, sanaa isisahaulike kwa sababu wataalamu wanaozalishwa wanahitajika kwa maendeleo ya nchi.

Vitu ambavyo hatasahau

Jambo ambalo atalikumbuka katika miaka yote aliyohudumu kama Mtakwimu Mkuu wa Serikali ni sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, ambayo ilimtesa yeye na Serikali baada ya baadhi ya watu kukataa kuhesabiwa.

“Serikali imeshatenga fedha, sasa watu hawataki, hiyo changamoto ilikuwa ni kubwa sana. La kwanza namshukuru sana Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alitusaidia kupambana hadi watu wakakubali kuhesabiwa,” anasema.

Anasema pia viongozi wa dini walisaidia, na baadaye watu hao walikubali, na hatimaye idadi ya watu ilipatikana kwenye sensa hiyo.

“Sitasahau, tulikuwa hatuwezi kulala. Nilikuwa na hayati Amina Mrisho Said, Mungu amuweke mahali pema peponi, akiwa ndiye kamisaa wetu wa sensa. Waziri wetu wakati huo alikuwa Mkulo (Waziri wa Fedha na Mipango, Mustafa Mkulo). Kwa kweli, haikuwa kazi rahisi, lakini tuliweza kwa kudra ya Mwenyezi Mungu,” anasema.

Aidha, Dk Chuwa anasema katika sensa ya mwaka 2022, jambo ambalo hatalisahau ni ahadi aliyoitoa duniani kuwa Tanzania itatekeleza shughuli hiyo kwa kidijitali, yaani kwa kutumia vishikwambi.

“Wenzetu Rwanda walitumia simu za mkononi (katika sensa ya watu na makazi) na sisi tukasema tutakwenda kidijitali, lakini mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) walipambana tukapata vishikwambi na kufanya sensa yetu. Kwa kweli, sitaweza kusahau; tumeitangazia dunia kuwa tutahesabu kidijitali,” anasema.

Dk Chuwa anamshukuru Rais Samia na viongozi wengine kwa jitihada walizofanya ili kupata vishikwambi kwa ajili ya kufanya shughuli hiyo kidijitali, na hivyo kufanikiwa kuwahesabu Watanzania kwa asilimia 99.9 kwenye sensa hiyo.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake

Dk Chuwa anasema kwa kaulimbiu ya mwaka huu ya Siku ya Wanawake Duniani, “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji,” hakuna namna unavyoweza kukimbia mchango wa takwimu katika kaulimbiu hiyo.

Anasema hiyo inatokana na takwimu zinazohitajika katika kufikia uwezeshaji, na kwamba ili kulifanya hilo ni lazima wadau wapate takwimu mbalimbali, ikiwemo za nguvu kazi na upatikanaji wa mikopo.

Dk Chuwa anasema kiu yake ni kuona wigo wa nafasi ya wanawake katika fursa mbalimbali inaongezeka na kufikia asilimia 50 kwa 50.

Anasisitiza takwimu zilizopo, zinazohusu masuala mbalimbali ya kiuchumi na upatikanaji wa mikopo, zinatumiwa ipasavyo katika uwezeshaji wa wanawake.

Anasema Siku ya Wanawake ni muhimu na kutaka itumiwe kuungana kwa pamoja na kufikiria wanawake walipotoka, waliko sasa, wanakwenda wapi, na wanalenga nini katika siku zijazo.

“Kwanza, kuondokana na umaskini. Umaskini huu ninaouzungumza sio wa chakula wala wa nini, bali ni nini tumekosa? Kama ni kwenye elimu tumekosa nini? Kama ni kwenye biashara tumekosa nini? Hatuna umaskini wa kukosa kufanya biashara kwa sababu mikopo ipo. Ni sisi kubadilisha fikra zetu,” anasema.

Anasema iwapo wanawake na wasichana watabadilisha fikra zao, kila kitu kinawezekana kwa kuchapa kazi kwa nguvu, uadilifu, ubunifu, na kwa kutumia fursa za ndani na nje.

Aidha, Dk Chuwa anasema anachoomba ni amani na utulivu nchini ili watu waendelee na shughuli za maendeleo, ambazo haziwezi kufanyika kama nchi inavurugu.