Kabla wiki hii haijamalizika, Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) litamtambulisha nyota wa zamani wa Porto, West Ham United na timu ya taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’, Benni McCarthy kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo ‘Harambee Stars’.

McCarthy (47) amekubali kazi ya kuinoa Harambee Stars akichukua mikoba ya Engin Firat ambaye Harambee Stars ilifikia uamuzi wa kuachana naye mwishoni mwa mwaka 2024.
Kocha huyo anajiunga na Harambee Stars baada ya kukaa kwa miezi saba bila timu tangu alipoachana na Manchester United ambayo alikuwa akiitumikia nafasi ya kocha wa washambuliaji wakati huo ikiwa inanolewa na meneja Erik Ten Hag.
Kenya imekuwa na matumaini makubwa kwa McCarthy kwamba atairudisha Harambee Stars katika makali yake ya zamani hasa katika nyakati ambazo timu hiyo inakabiliwa na Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wchezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) mwezi Agosti mwaka huu ambapo Kenya itakuwa ni miongoni mwa waandaaji wake.

Lakini pia McCarthy anategemewa kutengeneza timu imara ya Kenya itakayoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 ambazo zitafanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda na pia kuiongoza katika mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026.
Uzoefu wa kutosha
McCarthy ana uzoefu wa kutosha wa soka la Afrika lakini pia kwenye taaluma ya ukocha ambao ameupata kuanzia akiwa mchezaji na hadi alipogeuka ufundishaji wa mchezo huo.

Kwa soka la Afrika, McCarthy ana uzoefu nalo kwa kuchezea klabu tofauti hapo nyuma kabla hajastaafu ambazo ni Cape Towns Spurs, Seven Stars na Orlando Pirates za Afrika Kusini lakini kwa nyakati tofauti amezifundisha Cape Town City na Amazulu ambazo zote ni za Afrika Kusini.
Mchezaji huyo mbali na timu hizo, amewahi pia kuzichezea Ajax Amsterdam, Celta Vigo, Porto, Blackburn Rovers na West Ham United.
Katika ukocha amezifundisha Hibernian, Sint-Truiden na baadaye Manchester United.

Ameichezea timu ya taifa ya Afrika Kusini kwa miaka 15 kuanzia 1997 hadi 2012 ambapo alipachika idadi ya mabao 31 katika mechi 79.
Mataji, tuzo za kutosha
Akiwa mchezaji, McCarthy amewahi kushinda mataji 13 tofauti huku kubwa zaidi likiwa ni la Ligi ya Mabingwa Ulaya ambalo alitwaa akiwa na Porto msimu wa 2003/2004.

Tuzo binafsi alizowahi kupata ni uchezaji bora na ufungaji bora wa fainali za Afcon 1998 ambazo pia aliteuliwa kuwemo katika kikosi bora cha mashindano.
Alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ureno msimu wa 2003/2004 na akawa mfungaji bora wa Kombe la Ureno 2005/2026.
Kufanya kazi na hawa
Inaripotiwa kwamba katika majukumu yake ya kuinoa Harambee Stars, Benni McCarthy atasaidiwa na Vasili Manousakis na Moeneeb Josephs.