Huyu ndiye anayeipa jeuri Berkane

Berkane. Kocha wa Simba, Fadlu Davids amesema kuwa wapinzani wao RS Berkane ni timu inayofungika lakini kazi kubwa inapaswa kufanyika hasa kukabiliana na mchezaji wao mmoja tishio.

Davids amesema kuwa tathmini ambayo wameifanya, imebaini ili kupata matokeo mazuri dhidi ya RS Berkane, ni lazima wawe na mbinu za ziada za kumzidi ujanja kipa Munir Mohammed wa wapinzani wao hao.

Kocha huyo amemtaja Mohammed kuwa ndiye mchezaji anayeshikilia ushindi wa Berkane na kama wataweza kutumia vyema udhaifu wake, watakuwa na nafasi kubwa ya kupata ushindi dhidi ya Berkane.

“Ni muhimu kwetu kuzitawala nafasi kwa mchezo. Tunaufahamu huu uwanja na kocha wao hivyo ni muhimu sana kwa wachezaji kuelekeza akili kwenye mchezo tu.

“Kipa wao (Munir) amekuwa mchezaji muhimu kwenye timu tangu aliposajiliwa. Tunatakiwa kucheza mechi hii kama michezo mingine. Hatutakiwi kufikiria nyakati kadhaa tu maana sio rahisi kukabiliana RS Berkane kwa staili hiyo,” amesema Davids.

Munir ndio kipa anayeongoza kwa kucheza idadi kubwa ya mechi kwenye mashindano hayo bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa (clean sheets) ambapo amefanya hivyo katika michezo nane.

Kipa huyo anaongoza pia kwa kuwa na wastani mzuri wa kuokoa hatari kwenye mashindano hayo akiwa na wastani wa kufanya hivyo akiwa na asilimia 84.6 na hadi sasa ameruhusu nyavu zake kutikiswa Mara mbili tu.

Davids pia amesema anamfahamu vyema kocha wa Berkane, Moine Chabaan kwa vile amewahi kukutana naye mara kadhaa.

“Kocha wa Berkane amefanya kazi kubwa tangu alipojiunga nayo kutokea Raja. Ni timu yenye uwezo kimbinu wa kuukabili mchezo na jambo la muhimu kwetu ni namna gani ya kupunguza makali yao.

“Uwanja wao una eneo zuri la kuchezea. Tunajua watakuja na kasi na nguvu kubwa katika dakika 45 za kwanza. Msimu huu timu yangu imeonyesha utayari wa kucheza katika viwanja vyenye ubora tofauti wa eneo la kuchezea,” amesema Davids.

RS Berkane na Simba zitakutana kesho Jumamosi, Mei 17, 2025 kuanzia saa 2:00 usiku kwa muda wa hapa Morocco sawa na saa 4:00 usiku kwa muda wa Tanzania na baada ya hapo timu hizo zitakutana katika mechi ya marudiano Mei 25, 2025 katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Mechi hiyo ya mkondo wa kwanza baina ya RS Berkane na Simba itachezwa katika Uwanja wa Manispaa ya Berkane.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *