
MABOSI wa Azam FC wameanza kusaka mbadala wa kiungo nyota wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayedaiwa kuwindwa na klabu mbalimbali za ndani na nje ya nchi, zikiwemo Yanga aliyowahi kuichezea, Simba na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Fei Toto aliyejiunga na kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam maarufu kama lambalamba, Juni 8, 2023 akitokea Yanga, mkataba wake na timu hiyo unaisha mwakani 2026 na inaelezwa huenda asiongeze mwingine ili akatafute changamoto sehemu nyingine.
Wakati hilo likiendelea, taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza kiungo mshambuliaji, Kenan Armel Kader Glougbe anayeichezea Djoliba AC ya kwao Mali ndiye anayeangaliwa kama mbadala wa Feisal, ikiwa nyota huyo ataondoka kikosini.
Glougbe anayecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji au winga zote mbili za kulia na kushoto kwa ufasaha, ni miongoni mwa wachezaji wanaofanya vizuri na tayari klabu mbalimbali za Mali na nje ya nchi hiyo zimeanza kufuatilia upatikanaji wake.
Nyota huyo aliyezaliwa Agosti 19, 2004, mbali na kuichezea Djoliba AC ila ameitumikia pia Yeelen Olympique ya kwao Mali, huku ikielezwa mabosi wa Azam wameanza kumfuatilia nyota huyo, licha ya ushindani mkubwa kutoka kwa timu mbalimbali.
“Kwa sasa hakuna mazungumzo kati ya Azam na uongozi wa mchezaji kwa maana ya menejimenti yake na klabu inayommiliki, japo taarifa hizo ni za kweli na zipo ila kinachosubiriwa ni Ligi ya Tanzania kumalizika kwanza,” kilisema chanzo chetu.
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema sio wakati sahihi, kwani hakuna ripoti yoyote ya benchi lao la ufundi iliyowasilishwa hadi pale Ligi Kuu itakapomalizika.
Fei Toto ndiye mchezaji aliyefanya vizuri zaidi kwa mwaka 2024 na kiungo huyo alichangia mabao 27 ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga 15 na kuasisti 12, akimpipa bao, Stephane Aziz KI wa Yanga aliyefunga 12 na kuasisti pia mengine tisa.
Kiwango bora cha nyota huyo kilimfanya kumaliza na mabao 19 ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita, akiwa ndiye mchezaji mzawa aliyeshika nafasi ya pili kwa wachezaji waliofunga mabao mengi zaidi, nyuma ya Stephane Aziz KI wa Yanga aliyefunga 21.
Pia, aliibuka mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), msimu uliopita baada ya Azam kufika fainali na kuchapwa kwa penalti 6-5, kufuatia suluhu (0-0), mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
Mbali na hilo, ila Fei Toto aliiwezesha Azam kurejea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 10, tangu mara ya mwisho kikosi hicho kiliposhiriki 2015, baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-2014.
Ubora wa nyota huyo na kitendo cha mkataba wake kubakisha mwaka mmoja, kinawavuruga viongozi wa timu hiyo kutokana na miamba mbalimbali kuhitaji saini yake, jambo linalowafanya kuanza kusaka mbadala mapema kama atashindwa kubaki kikosini.
Fei Toto hadi sasa katika Ligi Kuu akiwa na kikosi hicho cha Azam, amehusika katika mabao 17, baada ya kufunga manne na kuasisti mengine 13, akiwa ndiye mchezaji anayeongoza kwa asisti nyingi zaidi.
Msimu huu pekee, Azam ilimsajili beki wa kati, Yoro Mamadou Diaby kutokea Yeleen Olympique na kiungo, Franck Tiesse kutoka Stade Malien zote za Mali, jambo linalowapa jeuri ya kuamini huenda ikainasa saini ya, Kenan Armel Kader Glougbe.