
WIKI iliyopita Singida Black Stars iliripoti kuwa imemuuza mshambuliaji wake Mtanzania Selemani Mwalimu ‘Gomez’ kwenda Wydad AC ya Morocco.
Kwenye eneo la ushambuliaji, Gomez atakutana na upinzani kutoka kwa Mohamed Rayhi, raia wa Uholanzi ambaye ni chaguo la kwanza la kocha Rulani Mokwena.
Rayhi ndiye kinara wa ufungaji kwenye ligi hiyo maarufu kama Botola Pro 1 akiweka kambani mabao manane.
Awali, vigogo hao wa Afrika walituma ofa kwa straika wa Yanga, Clement Mzize ambapo wananchi hao walikataa ofa hiyo wakitahitaji iboreshwe ndipo ikaenda kwa Gomez.
Nyota huyo aliyekuwa Fountain kwa mkopo aliuzwa Wydad kwa zaidi ya Sh800 milioni kwa mkataba wa miaka minne.
Kinara huyo wa mabao wa Fountain akiwa nayo sita anakuwa Mtanzania wa nne kusajiliwa na klabu kutoka Morocco baada ya Simon Msuva (Wydad na Difaa El Jadida), Maka Edward (Moghreb Tetouan) na Nickson Kibabage (Youssoufia Berrechid na Difaa El Jadida).
Mtanzania huyo anapaswa kupambana kuwania namba kwenye kikosi hicho cha kocha Muafrika Kusini Mokwena ambaye alithibisha kuhusika kumsajili.
“Ana kipaji kikubwa, na napenda kufanya kazi na wachezaji wa aina hiyo, amesajiliwa akiwa bado kijana na huo ndio mpango wa Wydad,” alisema Mokwena akizungumza na vyombo vya habari nchini humo.