Huu ndiyo mwelekeo mpya wa TLP ya Lyimo

Ni zama mpya kwa chama cha TLP baada kuingia madarakani kwa mwenyekiti mpya, Richard Lyimo, mwenye maono, fikra, ndoto na matamanio tofauti na ya mtangulizi wake, Augustino Mrema ambaye alikiongoza chama hicho kwa zaidi ya miongo miwili na nusu.

Lyimo alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa TLP, Februari 2, 2025, katika uchaguzi uliotawaliwa na migogoro hadi kufikia hatua ya kufukuzana kwenye chama na wengine kufikisha malalamiko yao Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Mwananchi limefanya mahojiano na Lyimo, akieleza mwelekeo wa uongozi wake na mambo anayokwenda kuyatekeleza ndani ya chama hasa kipindi hiki Taifa linapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Lyimo anasema malengo ya TLP, kama chama cha siasa, ni kushinda nafasi nyingi za udiwani na ubunge katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Anasema licha ya kwamba ameingia madarakani akiwa na muda mchache wa kujiandaa na uchaguzi mkuu, bado anaona anayo nafasi ya kufanikiwa kushinda nafasi nyingi.

“Jambo kubwa zaidi ili chama chetu kishinde nafasi nyingi za udiwani na ubunge ni kuhakikisha naongeza idadi ya wanachama katika mikoa na ngazi ya kata kwa kuwa tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu utakaotengeneza njia kushika dola,” anasema.

Lyimo, ambaye ametumikia kama katibu mkuu na naibu katibu mkuu wa chama hicho kwa nyakati tofauti, anasema baada ya kushika nafasi hiyo anajipanga kuwafuata Watanzania, wanachama na wasiokuwa wanachama wawe tayari kukipigia kura chama hicho.

“Nia na madhumuni ya chama cha siasa ni kushika dola, kwa msingi huo tunayo kazi ya kuushawishi umma. Jambo ninalolipa msukumo ni kujenga mshikamano na umoja kwenda kuwaaminisha Watanzania kukiunga mkono chama chetu,” amesema.

Kuvunja usultani

Lyimo anaahidi kuondoa dhana ya urithi iliyotamalaki ndani ya chama hicho huku akidai kuna baadhi wanachama walioshika nafasi kwa muda mrefu ndani ya chama hicho na wanajiona wanahaki zaidi kuliko wengine.

“Kuna watu wako ndani ya chama wanajifanya kama viongozi lakini uwajibikaji hamna, sasa ili niweze kusafiri katika safari yangu ni lazima niweke watu waliopo tayari kufanya kazi kama ninavyofikiri kulingana na mawazo yangu,” anasema.

Kiongozi huyo anasema ndani ya chama hicho kuna ukiritimba wa madaraka uliotamalaki kwa baadhi ya makada wake, hivyo kama kiongozi, anakwenda kusafisha kwa kuzingatia katiba na taratibu za chama hicho.

“Chama kinaelekeza utaratibu wa kupunguza na kuongeza watu naamini nitakaochagua wanaweza kusimama kwenye nidhamu na kutekeleza dira ninayotaka,” amesema.

Mbali na mabadiliko ya viongozi, ameahidi kuongeza ari na morali ya watu ndani ya chama hicho ili waweze kukitumikia chama na kwenda maeneo mbalimbali kukijenga.

“Ilikuwa ni vigumu mtu kwenda mikoa mbalimbali lakini kwa sasa baada ya kuingia mawasiliano yameanza kuwa mazuri kikubwa ni kuongeza ari watu wawe na nguvu na kuvutiwa na chama chao na kukilinda kwa wivu mkubwa,” anasema.

Dira ya uongozi wake

Lyimo ambaye alihamia TLP mwaka 1995 akitokea NCCR Mageuzi, anaeleza kwamba dira ya uongozi wake ni moja, kupata ushindi, na hilo litawezekana kwa kuungana pamoja kujenga chama ili kufikia azma hiyo.

“Bila ushindi hatuwezi kuwa na chama cha siasa, dira yetu ni kuhakikisha tunashinda chaguzi zijazo,” anasema.

Anasema amekuwa hawaonekani majukwaani wakifanya mikutano ya hadhara kwa kuwa ana muda mchache tangu amechaguliwa, hivyo kwa sasa amejikita na viongozi wake kuweka mikakati.

“Tunaanda viongozi na kuhusu kuonekana majukwaani, swali hilo litajibiwa baadaye baada ya kutoa mikakati na kuanza kuzunguka kuwaeleza wananchi,” anasema.

Anasema wanachofikiria ni kuanza kuwajenga viongozi wa wilaya na mikoa kwa kufanya mikutano ya hadhara ambayo itawafikia watu wote.

“Tutawajenga miongozi wawe na moyo wafanye mikutano ya kuwafikia wananchi mapema kabla ya uchaguzi,” anasema.

Anavyo mkumbuka Mrema

Akimzungumzia Mrema aliyefariki dunia Agosti 21, 2022, Lyimo anasema anamkumbuka kama kiongozi mwanamageuzi aliyedumu kwenye chama kwa muda mrefu.

“Namkumbuka alipokuwa na wabunge wengi na ni mwanzilishi wa mageuzi na kakiongoza chama kuwa na wabunge,” anasema.

Anasema tangu alipohama naye kundi la kwanza kutoka NCCR Mageuzi, Mrema alikuwa kiongozi mbunifu na mwenye uwezo wa kuhamasisha jamii kukiunga mkono chama chake.

“Alikifanya chama kuwa na wanachama wengi, namkumbuka kwa hayo, siwezi kumsahau,” anasema.

Mchakato wa kutia nia

Akizungumzia mchakato wa kutia nia, Lyimo anasema chama hicho kinawakaribisha wanachama wake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Anasema wamefungua milango na wametoa wito kwenye mikoa yao ya chama hicho kwa kuwatangazia wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

“Tunahitaji wagombea nafasi za ubunge na udiwani ili mradi wawe wamekidhi sifa na vigezo lakini tumetangaza nafasi ya urais kwa wenye uwezo na nia ya kugombea,” anasema.

Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, anasema wanapoelekea kwenye uchaguzi mkuu, chama hicho kinaenda na falsafa ya uongozi mpya na kazi mpya.

“Tunaenda kwenye uchaguzi na kauli mbiu yetu inayosema ‘mambo yaliyokuwa zamani na yakadumaza chama hatuko nayo tena’. Tunafanya kazi ya kujenga chama na kukirudisha kwa wananchi waliokuwa wanakihitaji lakini walikaa kimya,” anasema.

Chama kugawanyika

Kuhusu makundi na migogoro ndani ya chama hicho, Lyimo anasema chanzo cha migogoro ndani ya taasisi hiyo ni kwa sababu ilikabidhiwa kwa watu ambao hawajui misingi ya chama.

“Chama hakijawahi kuwa na migogoro isipokuwa watu waliokabidhiwa walikuwa hawajui katiba ya chama chetu, watu hawa wamekuwa wakifikiria uendeshaji wa chama bila kutumia katiba, taratibu na kanuni zilizotungwa, labda na sheria za usajili wa vyama vya siasa,” anasema.

Lyimo anasema anaona huo si mgogoro kwa kuwa haukuhusisha kuvunjwa kwa katiba ya chama, ingekuwa shida kama ungekuwa umeanzia kwenye katiba ya chama hicho kwa mtu kunyimwa haki.

“Pamoja na kwamba unaweza kuitwa mgogoro lakini kazi yangu ni kuboresha Katiba watu wanaojua katiba nitafanya nao kazi lakini wasiojua utafanyaje nao kazi hawajui wanachotaka,” amesema.

Lyimo anasema katika kipindi chake cha miaka mitano hahitaji kuona migawanyiko ndani ya chama lakini hataki kufanya kazi na watu ambao hawajui Katiba kwa kuwa hawatajua haki zao.

Kutumiwa na CCM

Kuhusu madai ya baadhi ya vyama vya upinzani kututumika na chama tawala kuhalalisha mambo yake, Lyimo anasema hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa kuwa hajawahi kuwa katika mfumo huo wa kutumika.

“Siwezi kujua ni kwa namna gani vyama hivyo vinatumika, kama lipo liache liendelee kama linafaida, lakini kwangu sipo tayari kutumika kisiasa kwa sababu Watanzania wanataka kuona mwenyekiti anafanya nini,” anasema.

Lyimo anasema Katiba yao inaruhusu ushirikiano lakini si kutumika kwa maslahi ya chama kingine cha kisiasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *