Huu ndio uwanja mpya wa Singida BS

KLABU ya Singida Black Stars leo, Jumatatu imeandika historia mpya kwa kuzindua rasmi uwanja wake wa nyumbani hapa Mtipa unaotajwa kuwa wa kisasa zaidi katika mkoa wa Singida.

Uzinduzi huu umepambwa na mchezo wa kirafiki kati ya wenyeji, Singida Black Stars, na mabingwa wa kihistoria wa Tanzania, Yanga.

HUU NDIO UWANJA MPYA WA SINGIDA BLACK STARS ‘Airtel Stadium’ | YANGA KAZI ANAYO LEO?

Uwanja huu umejengwa kwa lengo la kuleta mapinduzi katika soka la Singida na Tanzania kwa ujumla ukiwa na nyasi bandia kama ilivyo Uwanja wa Azam na KMC Complex vya jijini Dar es Salaam.

Dimba hilo ambalo ujenzi wake ulianza miaka minne iliyopita, litatoa mazingira bora kwa mchezo wa kasi na pasi fupi, mfumo unaoendana na falsafa ya timu nyingi za kisasa.

ENEO LA KUCHEZEA NA MIUNDOMBINU

Kwa asilimia 100, eneo la kuchezea limekamilika, likiwa na nyasi bandia zinazozingatia viwango vya kimataifa vya FIFA.

Uwanja huu unaruhusu kutumika katika mazingira tofauti bila kujali hali ya hewa, kwani mifumo ya mifereji ya maji imewekwa kuhakikisha hakuna maji yanayotuama hata wakati wa mvua kubwa.

Tofauti na viwanja vingine nchini, uwanja wa Singida una uzio wa kisasa wa nyavu imara zinazozuia mashabiki kuingia uwanjani kiholela. Ulinzi huu unatoa usalama kwa wachezaji na waamuzi.

MAJUKWAA NA SEHEMU ZA MASHABIKI

Licha ya kwamba uwanja unazinduliwa rasmi leo, bado ujenzi unaendelea, hasa upande wa majukwaa ya mashabiki.

Kwa sasa, sehemu ya VIP pekee ndiyo imewekewa viti, huku maeneo mengine yakitarajiwa kufanyiwa maboresho ili kuwa na mkao bora kwa mashabiki wengi zaidi.

Kwa ukubwa wake, uwanja huu unaweza kuwa moja ya viwanja muhimu kwa mashindano mbalimbali nchini.

Singida Black Stars inatarajia kuutumia kama wa nyumbani kwa mechi zote za Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ikiufanya kuwa sehemu ya maendeleo ya soka mkoani hapa.

VYUMBA VYA KUBADILISHIA NGUO

Sehemu ya vyumba vya kubadilishia nguo tayari imekamilika, ikiwa na nafasi kubwa, sehemu za kuogea, na vifaa vyote muhimu kwa maandalizi ya wachezaji kabla na baada ya mechi.

Mfumo wa hewa safi umezingatiwa ili kuwafanya wachezaji wawe kwenye hali nzuri wanapojiandaa kwa michezo yao.

Kwa upande wa huduma kwa mashabiki na wageni wa uwanja, bado ujenzi wa vyoo unaendelea. Menejimenti ya Singida Black Stars imeeleza kuwa vyoo vya kisasa vinajengwa ili kuendana na hadhi ya uwanja huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *