
Katika ulimwengu wa leo ambapo vyakula vilivyosindikwa vimejaa katika masoko na majumbani mwetu, ni muhimu kwa watu wenye kisukari kuelewa faida za kula wanga asilia hasa vya mizizi kama maboga, magimbi, viazi vikuu na mihogo.
Wanga huu wa asili una faida nyingi kiafya, kwani husaidia kudhibiti kiwango cha sukari mwilini na kutoa nishati ya kudumu kwa mwili.
Tofauti na wanga uliosindikwa unaopatikana kwenye vyakula kama mikate, biskuti na vyakula vya ngano, wanga asilia kutoka kwa mizizi una kiwango cha chini cha sukari.
Hii inamaanisha kuwa haupandishi kiwango cha sukari mwilini kwa haraka, hivyo kusaidia katika kudhibiti kiwango cha sukari kwa watu wenye kisukari.
Magimbi na viazi vikuu vina nyuzinyuzi nyingi ambazo hupunguza kasi ya usagaji wa wanga mwilini, hivyo kuzuia viwango vya sukari kupanda kwa haraka.
Hii ni faida kubwa kwa watu wenye kisukari wanaotakiwa kudhibiti viwango vyao vya sukari kila siku.
Watu wenye kisukari wanapaswa kula vyakula vinavyowapatia nishati ya kudumu bila kuathiri afya zao. Mizizi kama mihogo, magimbi na maboga ni chanzo bora cha nishati inayotolewa kwa utaratibu mzuri mwilini.
Hii inasaidia kuepuka hali ya uchovu wa ghafla unaoweza kusababishwa na kushuka kwa sukari mwilini.
Vyakula hivi husaidia katika kuimarisha utendaji kazi wa mwili, hivyo kuwapa wenye kisukari nguvu za kushiriki katika shughuli za kila siku bila kuhisi uchovu haraka.
Maboga, viazi vikuu na magimbi pia vina virutubisho muhimu kama vitamini, madini na nyuzinyuzi.
Maboga yana vitamini A inayosaidia kuboresha afya ya macho, magimbi yana madini ya chuma yanayosaidia kupunguza hatari ya upungufu wa damu, huku mihogo ikiwa na vitamini C ambayo inasaidia kuongeza kinga ya mwili.
Nyuzinyuzi zinazopatikana katika vyakula hivi husaidia pia katika usagaji wa chakula na kupunguza kiwango cha lehemu mbaya mwilini, hivyo kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo ambayo ni miongoni mwa matatizo yanayoweza kumpata mtu mwenye kisukari.
Watu wenye kisukari wako kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa mbalimbali hasa kwa wale ambayo viwango vyao vya sukari kuwa juu mara kwa mara.
Kula vyakula vya mizizi vyenye vitamini na madini husaidia kuimarisha kinga ya mwili na kuzuia maambukizi. Kwa mfano, maboga yana vioksidishaji ambavyo hupunguza madhara ya sumu mwilini na kusaidia mwili kupambana na magonjwa.
Watu wenye kisukari wanaotafuta mbadala wa vyakula vya ngano na wali vilivyosindikwa, kwao mizizi kama mihogo, viazi vikuu na magimbi ni suluhisho sahihi.
Vyakula vya aina hii vinaweza kupikwa kwa njia mbalimbali kama kuchemsha, kuchoma au kukaanga bila mafuta mengi ili kuepuka ongezeko la mafuta.