
Dar es Salaam. Ndoa ni muungano wa maisha kati ya wanandoa unaotarajiwa kudumu kwa muda mrefu maishani. Ni muungano ambao kimsingi hupaswa kukoma pale mmoja anapofikwa na umauti,
Ndio sababu watu wanapofunga ndoa hula kiapo cha kukubali kuishi kwa mazuri na mabaya hadi kifo kiwatenganishe.
Hata hivyo, hali haiko hivyo, ongezeko la talaka nchini linatisha. Takwimu za Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke, zinaonyesha kati ya Novemba 2021 hadi Julai 2023, kulikuwa na mashauri ya ndoa na talaka 1358 yaliyoripotiwa. Idadi hiyo ni sawa na mashauri 220 yanayoripotiwa kituoni hapo kila mwezi.
Talaka uzeeni
Hata hivyo, wakati talaka nyingi zikitajwa kuhusisha vijana ambao wengi huingia kwenye ndoa kama wanafanya majaribio au kwa kukosa maarifa sahihi ya ndoa, lipo wimbi pia la watu waliokula chumvi nyingi kuachana.
Ipo mifano ya watu maarufu duniani walioachana wakiwa na umri mkubwa.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na mkufunzi wa masuala ya saikolojia kutoa Chuo Kikuu cha Bowling Green State cha nchini Marekani, Susan Brown mwaka 2022 na kuchapishwa katika jarida la The Journals of Gerontology, asilimia 36 ya talaka zinazotokea wanandoa katika umri mkubwa, huanzia miaka 50 na kuendelea.
Said Suleiman (60) ambaye ni baba wa watoto watano anasimulia namna alivyoachana na mkewe baada ya kuishi pamoja kwenye ndoa kwa takribani miaka 25.
Suleiman anasema safari yake ya maisha kati yake na mkewe ilianza miaka 30 iliyopita baada ya kufunga ndoa mwaka 1995 wakiwa tayari wamebahatika kupata mtoto mmoja.
Anasema maisha yao ya ndoa yaliyodumu kwa zaidi ya miongo miwili yalikwenda vizuri licha ya kutokea changamoto za hapa na pale.
Hata hivyo, anasema baada ya ndoa yao kufikikisha miaka 24 mkewe alianza kumlazimisha kumpa talaka, huku akimtuhumu kuwa na mwanamke mwingine.
“Alianza kunifanyia visa akisema amegundua kuwa na nina mwanamke mwingine hadi kusababisha kuhama nyumbani. Mwisho niliona kama mapenzi yamekwisha nikaona nimkubalie takwa lake la talaka na kuachana rasmi mwaka 2020, ”anaeleza.
Ukiachana na Suleiman, Kisa Mwenda ambaye ni mama wa watoto watatu na bibi wa wajuu wawili, naye anasimulia namna alivyofanya maamuzi ya kuomba talaka na kuachana na mwenza wake wakiwa tayari wameshakula chumvi nyingi.
Anasema chanzo cha kufikia uamuzi huo, ni baada ya mumewe kustaafu na kupata mafao yake alibadilika na kuanza tabia ya ulevi.
“Alianza kuwa mlevi kupindukia, hakujali tena kuhusu mke wala familia. Niliendelea kuvumilia nikiamini atabadilika lakini hilo halikutokea, ikanilazimu kuomba kukaa kando, ”anasema.
Makovu ya maumivu yaliyotokea ujanani
Akizungumza na Mwananchi, mwanasaikolojia, Modesta Kimonga anasema moja kati ya sababu zinazochangia wanandoa kupeana talaka baada ya kuishi kwa miongo kadhaa, ni pamoja na makovu ya maumivu aliyosababishiwa na mwenza wake wakati wa ujana, sababu za kiafya, kutokuwepo kwa uvumilivu, mabadiliko mbalimbali ya mwili pamoja na msongo wa mawazo katika umri mkubwa.
Kimonga anasema katika maisha ya ndoa, wenza hufanyiana mambo mengi yakiwmao yale mabaya.
Anasema inawezekana katika maisha yao ya ndoa enzi za ujana, mwanamke au mwanaume aliwahi kumfanyia mweza wake tukio fulani baya kwa mara kadhaa.
“Lakini mwenziwe akavumilia na kuacha maisha yaendelee kwa kuwa wameishi kwa muda na wana watoto, huku moyoni na akilini mwake akiendelea kuishi na taswira mbaya pamoja na makovu ya maumivu jambo ambalo halina afya kwa ustawi wa uhusiano, ”anasema.
Anaeleza kuwa ikitokea matendo hayo mabaya aliyoyafanya mwenza kwa mwenzie wakati wa ujana yakijirudia kipindi cha uzee na kuendelea kuota mizizi, yanaweza kumfanya akachoka kuvumilia na kufikia uamuzi wa talaka.
“Ikiwa matatizo kama vile usaliti kipindi cha nyuma ugomvi wa mara kwa mara, au ukosefu wa heshima katika ndoa hayakupatiwa ufumbuzi mwishowe husababisha talaka hata baada ya miaka mingi ya ndoa, ”anaeleza.
Mabadiliko ya kimwili, kiakili na kihisia
Kimonga anasema kadri umri unavyosonga, watu hubadilika kimwili, kiakili, na kihisia. Wengine wanapofikia uzee hupitia changamoto kama magonjwa sugu, kupungua kwa nguvu za mwili au hata kubadilika kwa mtazamo wa maisha.
Anatolea mfano baadhi ya watu wanapofikia umri wa uzee, hupata maradhi mbalimbali ikiwemo kisukari, presha, maumivu ya mgongo na mengine na kusababisha kushuka kwa ufanisi wake katika utendaji wa mambo mbalimbali.
Pia anasema pamoja na watu wa umri huo kuwa katika hatari ya kupata magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza, huweza kupitia mabadiliko mbalimbali ya lazima katika miili yao.
Anasema baadhi ya wanawake wanapofika katika kipindi cha ukomo wa hedhi au kufikia umri wa uzee, wanapitia mabadiliko mbalimbali ya kimaumbile na kihisia, ambayo kama mwenza asipokuwa mvumilivu na mwelewa yanaweza kusababisha migogoro katika ndoa na hatimaye talaka.
“Ikiwa wanandoa hawako tayari kukabiliana na mabadiliko haya pamoja, huenda wakahisi kutotoshelezwa na wenzao, hivyo kuamua kutalikiana, ”anaeleza.
Kukosekana kwa uvumilivu
Kimonga anasisitiza kuwa moja kati ya nguzo muhimu ya kudumisha ndoa ni uvumilivu.
Anasema maisha ya kwenye ndoa katika kipindi cha ujana, hutofautiana na ya wakati wa uzee kutokana na mabadiliko na changamoto mbalimbali zinazojitokeza.Hivyo ili kukabiliana na kuvuka hali hiyo, kunahitaji wenza kuwa na uvumilivu.
“Wenza wakishindwa kuwa wavumilivu na kusameheana katika kipindi hicho cha uzee, wanaweza kusababisha kupungua kwa upendo miongoni mwao. Upendo ukipungua kunaweza kuzalisha migogoro ya mara kwa mara ambayo isipopata tiba wanaishia kutalikiana,”anaeleza.
Suluhu ya talaka za uzeeni
Mtaalam na mshauri wa masuala ya uhusiano, Eva Mrema anasema ili wanandoa wajiepushe kutalikiana wakati wa uzeeeni, wanapaswa kuzungumza waziwazi kuhusu hisia, matarajio, changamoto wanazokumbana nazo, kuepuka kinyongo na kuzungumza kwa uwazi.
Eva anasema kama njia ya mazungumzo kati yao ikishindikana, ni vyema kutafuta msaada kutoka kwa mshauri wa ndoa au kiongozi wa kidini.
“Ushauri wa kitaalamu unaweza kusaidia kutatua tofauti kwa njia ya amani, ”anaeleza.
Pia anachombeza kuwa wenza hao japokuwa wana umri mkubwa, lakini wasiache kufanya yale mambo madogo madogo ambayo husaidia kunogesha uhusiano kama vile kushikana mikono, kukumbatiana na kusifiana, akisema yanasaidia kudumisha hali ya kimapenzi na kuzuia hisia za kutojali.
“Kushiriki shughuli kama vile matembezi, safari, au kupata muda wa kufurahia pamoja, husaidia kuimarisha uhusiano wa kimapenzi,’’ anashauri.
Anasema katika safari ya maisha, wenza wanaweza kufanya makosa mbalimbali, hivyo badala ya kuyahifadhi moyoni, ni bora kusamehe na kuendelea mbele kwa pamoja.
Anaongeza kuwa suala la uvumilivu ni muhimu katika kudumisha ndoa kwani ndoa ni safari inayohitaji bidii na uvumilivu, huku matunda yake yakiwa furaha ya milele.