Human Rights Watch yakiri kuhusika utawala wa Kizayuni wa Israel na jinai za kivita

Katika ripoti yake ya hivi karibuni zaidi, shirika la kuteteta haki za binadamu la Human Rights Watch kwa mara nyingine tena limetangaza kuwa utawala haramu wa Israel umefanya jinai za kivita dhidi ya binadamu na mauaji ya kikabila huko Gaza, kuharibu vyanzo vya maisha na kuwafanya kuwa wakimbizi mara kadhaa asilimia 90 ya wakaazi wa Gaza.

Shirika hilo limeeleza kuwa madai ya Israel kuhusu kuwapa makazi upya watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza ni uongo mtupu, na kuongeza kuwa hakuna sehemu yoyote iliyobakia salama ndani ya Gaza kwa sababu jeshi la utawala huo linashambulia mara kwa mara maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wakimbizi.

Vita huko Gaza vinaendelea huku jinai za Israel katika eneo hilo zikiathiri kwa njia mbalimbali haki za binadamu ambapo Wapalestina milioni mbili wanaoishi katika ukanda huo wanakabiliwa na changamoto kubwa za kudhamini usalama, chakula, afya na miundombinu muhimu ya kuendeleza maisha.

Kuhusiana na hilo, taasisi za kimataifa zimekuwa zikionya mara kwa mara kuhusu uharibifu mkubwa uliofanywa na Israel kwenye miundombinu, mifumo ya uchumi na uhaba mkubwa wa mchakula, maji na dawa katika Ukanda wa Gaza.

Anna Halford, mratibu wa masuala ya dharura katika Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, amesema: “Israel imefanya jinai ya kivita ya kuwaadhibu watu kwa pamoja dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, ambapo sasa wakazi wa kaskazini mwa ukanda huo wanalazimika kuchagua moja kati ya machaguo mawili; ima kuuawa au kuhamishwa kwa lazima.”

Jinai za Israel dhidi ya Wapalestina

Kwa hakika utawala wa Kizayuni ambao umeshindwa katika vita vya Gaza licha ya kutumia suhula  na silaha zote za kisasa dhidi ya Wapalestina, umekuwa ukijaribu kuwafanya Wapalestina waliobakia huko walazimike kukimbia au wauawe kwa kuzidisha mzingiro wa kikatili dhidi yao.

Louis Waterridge, afisa mkuu katika shirika la UNRWA ambaye amekuwa akihudumu Gaza kwa muda wa miezi sita iliyopita, amesema kuhusu suala hili: “Mashambulio ya mabomu pia hayaelezeki.Unaamka asubuhi, labda una makazi, chakula na tenki la maji, lakini ghafla bomu linalipiga na unapoteza kila kitu au unakuwa mkimbizi. Kuhamishwa ni kwa kikatili kama ilivyo milipuko ya mabomu. Mara tu familia inapotulia mahali fulani pa kukaa kwa muda ghafla hupokea onyo la kuondoka hapo na kuhamia kwingine.”

Kamati Maalum ya Umoja wa Mataifa pia imekiri katika ripoti iliyochapishwa muda mfupi uliopita kwamba: “Mbinu za vita zinazotumiwa na Israel katika Ukanda wa Gaza ni sawa na mauaji ya halaiki ambapo inatumia njaa kama silaha ya vita.”

Nadia Hardman, mtafiti katika Idara ya Haki za Wakimbizi na Wahamiaji katika shirika la Human Rights Watch, anasema kuhusiana na suala hili kwamba: “Israel haiwezi kudai kuwa imewadhaminia Wapalestina usalama wao huku ikiendelea kuwaua kwa umati barabarani na wanapojaribu kukimbia vita, kulipua kwa mabomu maeneo yanayodaiwa kuwa ni salama na kuzuia chakula, maji na vifaa vya afya kuingia Gaza. Kwa hakika, Israel imekiuka wazi wajibu wake wa kuhakikisha wakimbizi wa Palestina wanarudi katika makazi yao kwa sababu imelipua na kuyabomoa yote.”

Utawala wa Kizayuni unaendeleza jinai zake dhidi ya Wapalestina wa Gaza kwa uungaji mkono kamili wa nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, licha ya malalamiko yote ya kimataifa, ripoti na maombi ya taasisi za kimataifa ya kuutaka usimamishe mara mnoja jinai zake dhidi ya watu wasio na hatia. Nchi hizo ambazo daima hudai kutetea haki za binadamu na uhuru, zimekuwa waungaji mkono wa pande zote wa Israel katika jinai hizo bila ya kujali lolote. Kwa kadiri kwamba zinaendelea kutoa misaada ya kila aina kwa utawala huo licha ya ripoti za kimataifa kwamba utawala huo unahusika moja kwa moja na mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina. Gazeti la kiuchumi la Globes la utawala wa Kizayuni limeandika kuwa, Wizara ya Vita ya utawala huo tangu kuanza kwa uvamizi wake katika Ukanda wa Gaza mnamo tarehe 7 Oktoba 2023 hadi sasa; imetia saini mikataba ya kijeshi yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 40 na Marekani na pia kupokea msaada wa kisiasa na kijeshi kutoka kwa nchi hiyo ya Magharibi.

Uharibifu wa makusudi wa Israel dhidi ya makazi ya Wapalestina

Hii ni katika hali ambayo Vedant Patel, Naibu Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema kuhusiana na hili kwamba hata kama Marekani haikubaliani na siasa za vita za Israel kwa sasa lakini itaendelea kuiunga mkono na kuisadia kwa hali na mali.

Kwa hivyo, utendaji wa nchi za Magharibi hususan Marekani kwa jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina unaonyesha kuwa licha ya ripoti mpya ya shirika la Human Rights Watch kuhusu ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu na jinai za kivita zinazofanywa na Israel huko Gaza, lakini nchi hizo zimeamua kuendelea kuunga mkono siasa za mauaji ya umati na jinai za kivita za utawala huo wa kibaguzi huko Gaza.